Zahera alalamikia muda wa mechi

Muktasari:

  • Yanga inacheza mchezo wake dhidi ya Mtibwa Sugar leo Jumatano saa nane mchana.
  • Pia timu hiyo inashuka dimbani ikiwa imekusanya pointi 74 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

KOCHA wa Yanga, Mwinyi Zahera amesikitishwa na bodi ya ligi TBL kubadilisha muda wa kucheza mechi yao na Mtibwa Sugar kutoka saa 10:00 jioni hadi saa 8:00 mchana kwamba inawaumiza wachezaji wao.
Shirikisho la Soka Tanzania Bara (TFF), jana kupitia kwa msemaji wake  Clifford Ndimbo walitoa taarifa ya kurudisha nyuma muda wa kucheza mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Simba na Coastal Union (Mkwakwani).
Kitendo hicho kimemuumiza kocha Zahera aliyedai wachezaji ni binadamu wanapaswa kuangaliwa wnapopanga mechi zao kujua maumivu ambayo wanayapata.
"Wachezaji sio chungwa wala mbuzi ni binadamu, haiwezekani mechi kutoka saa 10:00 jioni kuirudisha nyuma mpaka saa 8:00 hali ya hewa inakuwa inawaumiza kupita kiasi.
"Kama ni michuano ya AFCON kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 ambayo Tanzania ni wenyeji ratiba yao ilikuwa inajulikana tangu mwanzo, inapotokea haya inaumiza.
"Ushauri wangu upangaji wa ratiba uzingatie na afya za wachezaji pia wanaumia kwa kuwa wanatumia damu"anasema.
Naye kocha wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amesema wapo tayari kupambania pointi tatu, huku akisisitiza kwamba dakika 90 ndizo zitaamua nani kachanga kalata yake vyema.
"Mechi ni ngumu Yanga ni timu kubwa na ina wachezaji wazoefu, kikosi changu pia kina wachezaji wapambanaji ni mechi ngumu dakika 90 zitaamua matokeo"anasema.