Yondani, Fei Toto kuikosa Rwanda, hatihati kuivaa Sudan

Muktasari:

Stars itavaana na Rwanda kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa kabla ya kwenda Sudan kurudiana na wenyeji wao waliowalaza bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya kuwania fainali za Chan zitakazofanyika Cameroon.

Dar es Salaam. KIKOSI cha Timu ya Taifa, Taifa Stars kipo mjini Kigali Rwanda kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya Rwanda, lakini kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na beki Kelvin Yondani ‘Corton Juice’ wamekitibua baada ya kukwama kuambatana na timu hiyo inayowania kucheza Fainali za Chan 2020.
Stars itavaana na Rwanda kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa kabla ya kwenda Sudan kurudiana na wenyeji wao waliowalaza bao 1-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya kuwania fainali za Chan zitakazofanyika Cameroon.
Hata hivyo, Yondani na Fei Toto wanaokipiga Yanga, wameshindwa kuambatana na timu hiyo kwa sababu mbalimbali na kuzua utata kwa mashabiki wa soka.
Kocha Mkuu wa Stars, Etienne Ndayiragije alisema amesafiri na nyota wake wote waliokuwa wameingia kambini isipokuwa Fei Toto ambaye amekwama kutokana na kukosa pasipoti ya kusafiria.
“Tumeshawafika salama  Rwanda na nyota 28 ni mchezaji mmoja tu amebaki Tanzania aliyeshindwa kusafiri nasi ambaye ni Fei kutokana na kukosa pasipoti ya kusafiria,” alisema, huku suala la Yondani ikibainika amekwama kwa vile ni majeruhi.
Fei Toto alikiri ni kweli amekwama kuondoka na timu hiyo kwa sababu ya hati ya kusafiria (pasipoti).
“Nina pasipoti ya zamani ambayo kwa Rwanda ninaweza kuingia, ila timu ikitoka hapo itaunganisha kwenda Sudan ambako siwezi kuingia nayo,” alisema Fei Toto na kuongeza: “Pia nina matatizo ya kifamilia yananikabili kwa hiyo vipo vitu vingi ambavyo vimenifanya nishindwe kuambatana na timu yangu ya taifa.”
Jambo hilo la Fei kukosa pasipoti limezua utata kwani Ditram Nchimbi aliyeitwa hivi karibuni ikielewa kwamba hakuwa na hati hiyo lakini ameshaipata ndani ya muda mfupi, lakini sababu hiyo aliyoitoa Fei na ikizingatiwa ni jukumu la kitaifa limefanya watu wahoji imekuwaje suala la kiungo huyo lishindwe kutatuliwa mapema.
Hata hivyo, Ofisa Habari wa Uhamiaji, Ally Mtanda alipotafutwa kuelezea suala la pasipoti ya zamani kukwamisha mchezaji anayeitumikia taifa kutomruhusu kuingia Sudan, alifafanua akisema nchi zote zilizo Afrika Mashariki pasipoti za zamani zinatumika.
“Inafuatana na mtumiaji huyo wa paspoti anaenda Sudan ya ipi, ya Afrika Mashariki anaweza kuingia isipokuwa kama ataenda katika nchi inayotumia Visa hawezi kuruhusiwa na kama ni mchezaji anakithibitisho cha uharaka wa kupata paspoti anaweza kushughulikiwa kwa uharaka,” alisema Mtanda.
Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema ni kweli Fei amekwamishwa na hati ya kusafiria baada ya kuchelewa kushughulikiwa, japo hana hakika kama ataungana na wenzake Sudan kama itapatikana kwa haraka kuwahi mechi ya Oktoba 18.
“Ni kweli Fei alikuwa na tatizo la pasipoti, yake ni ya zamani na ili agongewe viza ilipaswa isiwe chini ya miezi sita, ila yake imevuka na sio yeye tu kuna wenzake waliokuwa na tatizo kama lake, ila yake imechelewa kutoka na inashughulikiwa.”
Kuhusu Yondani, Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema Yondani hajaondoka kwa vile anasumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu alichoumia kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union.
“Viongozi tulitoa ruhusa ya kuungana na kikosi cha timu ya taifa lakini alishindwa kufanya hivyo kwa kutoa taarifa kuwa bado anasumbuliwa na tatizo alilolipata kwenye mchezo wa ligi,” alisema Hafidh.