Yanga yazidi kunoga

Muktasari:
Ngassa ambaye aliisaidia Yanga kubeba taji lao la 25 la Ligi Kuu msimu uliopita alikuwa miongoni mwa wachezaji walioshiriki mazoezi hayo ya Yanga kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, huku wakali wengine waliokosekana mwanzoni wakitia timu kimtindo.
KIKOSI cha Yanga kinachoendelea kujifua kujiandaa na michuano ya Kombe la Kagame na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara, kimeanza kunoga baada ya idadi ya wachezaji wake kuzidi kuongezeka, huku winga wao wa zamani Mrisho Ngassa akitua kuwapiga tafu kiaina.
Ngassa ambaye aliisaidia Yanga kubeba taji lao la 25 la Ligi Kuu msimu uliopita alikuwa miongoni mwa wachezaji walioshiriki mazoezi hayo ya Yanga kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, huku wakali wengine waliokosekana mwanzoni wakitia timu kimtindo.
Baadhi ya wachezaji walioongezeka kwenye mazoezi hayo ya jana Jumatatu, mbali na Ngassa aliyesajiliwa Free State Stars ya Afrika Kusini ni saba ambao ni wale waliokuwa kwenye vikosi vya timu za taifa za Tanzania, Rwanda na Burundi.
Wachezaji hao ni pamoja na Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Amissi Tambwe, Deus Kaseke, Malimi Busungu na Salum Telela, ambao waliungana na wachezaji waliokuwa awali tangu kuanza kwa mazoezi hayo wiki mbili zilizopita na kumpa raha kocha Hans Pluijm.
Walioanza mapema mazoezi hayo ni pamoja na Benedictor Tinocco, Ally Mustapha ‘Barthez’, Geofrey Mwashiuya, Andrey Countinho, Kpah Sherman, Hussein Javu, Rajab Zahir, Joseph Mapembe na Kelvin Yondani, huku Msierra Leone, Lansana Kamara akikosekana kwa jana.
Akizungumzia uwepo wake katika mazoezi hayo, Ngassa alisema anafanya mazoezi na Yanga kwa ajili ya kujiweka fiti kabla ya kwenda kufanya kazi yake Afrika Kusini na kwamba aliamua kuichagua timu hiyo kwa sababu ni timu aliyoizoea, mabingwa na anajihisi kama yuko nyumbani kwake.
KADUGUDA NAYE
Mbali na ujio wa Ngassa katika mazoezi ya jana pia Katibu Mkuu wa zamani wa Simba, Mwina Kaduguda naye alitia timu kuyacheki mazoezi hayo, ingawa alienda uwanjani hapo kwa kazi maalumu.
Kaduguda aliyekuwa akizungumza na Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Tiboroha alipoulizwa juu ya uwepo wake katika mazoezi hayo alisema yupo kwa ajili ya kuandaa kitabu chake tu na pia alizungumzia kuhusu mfumo wa soka la Tanzania akidai unachangia kuifanya Stars kuwa nyanya.
“Timu ya Taifa kufanya vibaya sababu ni mfumo wetu wa soka, ni mbovu na pia tunaamini kuwa mwenye pesa ndio kiongozi lakini tunajidanganya kiongozi ni yule anayejua mpira.”