Yanga yazichochea Simba, Azam kimataifa

Muktasari:
Kufuzu hatua hiyo kutaifanya Yanga ijihakikishie kitita cha Dola 275,000 (zaidi ya Sh 630 milioni) ambazo hutolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa timu inayotinga hatua hiyo.
YANGA imeondolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia Kombe la Shirikisho ambako itacheza mchujo kusaka nafasi ya kutinga hatua ya makundi.
Droo ya mechi hizo inatarajiwa kufanyika Oktoba 9 na Yanga kujua itavaana na nani kabla ya kupenya makundi ambapo kama itafanya hivyo itakuwa mara yao ya tatu baada ya 2016 na 2018.
Kufuzu hatua hiyo kutaifanya Yanga ijihakikishie kitita cha Dola 275,000 (zaidi ya Sh 630 milioni) ambazo hutolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kwa timu inayotinga hatua hiyo.
Fedha hizo zitaongezeka na Yanga ikapata kiasi kikubwa zaidi ikiwa itavuka na kutinga hatua za juu zaidi za Robo Fainali, Nusu Fainali na hata kubeba ubingwa.
Lakini, wakati Yanga ikizisaka fedha na heshima binafsi kwenye Shirikisho, wawakilishi hao wa nchi wana kibarua kingine kigumu cha kulinda nafasi ya Tanzania kuingiza klabu nne kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu ujao.
KAZI IPO HAPA
Baada ya Tanzania kuneemeka na uwakilishi wa timu nne katika michuano ya Afrika msimu unaoendelea, kama Yanga isipokaza buti na kutinga hatua ya makundi na pia huko ikafanya vizuri, ni wazi kwamba msimu ujao Tanzania itarudi katika maisha ya kawaida ya kuwakilishwa na timu mbili tofauti na msimu wa sasa.
Tanzania imeingiza timu nne msimu huu kutokana na kuwa miongoni mwa nchi 12 ambazo zimekusanya idadi kubwa ya pointi kulingana na ushiriki na ufanisi wa timu zao kwenye mashindano ya klabu Afrika.
Pointi huhesabiwa kutokana na nafasi ambayo klabu ya nchi husika imemaliza katika michuano hiyo ya Afrika ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Msimu huu, Tanzania imeingiza timu nne kwani katika misimu mitano iliyopita kuanzia 2015, 2016, 2017, 2018 na 2018/2019 ilikusanya jumla ya pointi 18 na kushika nafasi ya 12.
Pointi hizo 18, zilitokana na pointi moja ya mwaka 2016 iliyotokana na kitendo cha Yanga kumaliza nafasi ya tatu kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ambapo ilipatiwa alama 0.5 iliyozidishwa na namba ya mwaka husika iliyokuwa mbili (2).
Pointi hiyo moja ilijumlishwa na nyingine mbili (2) ambazo Yanga ilizipata kwa kushika nafasi ya tatu katika hatua ya makundi ya Shirikisho 2018 ambayo ilipatikana kwa kuzidisha 0.5 kwa alama ya mwaka 2018 iliyokuwa ni nne (4).
Na kwa vile Simba ilifikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, ilipata pointi tatu ambazo zilizidishwa kwa alama tano (5) ikiwa ni ya msimu uliopita na kupatikana jumla ya pointi 15 zilizojumlishwa na pointi tatu zilizokusanywa na Yanga kwa 2016 na ule wa 2018 kupata jumla ya pointi 18.
Hata hivyo, kwa vile ukokotoaji huo hutazama mafanikio ya klabu za nchi husika kwenye kipindi cha miaka/misimu mitano nyuma, ili kupata timu za msimu ujao, hesabu hizo zitapigwa kwa kuanzia ushiriki wa timu kwenye msimu wa mwaka 2016.
Maana yake, alama 0.5 ambazo Yanga ilizipata mwaka 2016, hazitozidishwa kwa mbili bali moja na kupata pointi 0.5, alama kama hiyo ambayo Yanga ilipata mwaka 2018 itazidishwa kwa tatu 3) na sio nne (4) kama ilivyokuwa msimu uliopita na zitapatikana pointi 1.5 badala ya 2 zilizotumika kwa msimu huu na pia alama 3 ambazo Simba ilizipata kwa kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, haitozidishwa tena kwa tano bali nne na kufanya jibu liwe pointi 12 na sio 15 kama ilivyokuwa kwa msimu huu.
Kwa hesabu hizo, pointi za Tanzania zitapungua kutoka 18 ilizonazo sasa hadi 14 na hivyo inaweza kujikuta ikiondolewa kwenye kundi la nchi 12 zinazotoa wawakilishi wanne kwenye mashindano ya Afrika kila moja hasa baadhi ya nchi zilizokuwa chini yake zikifanikiwa kuongeza idadi ya pointi kutokana na kufanya vizuri kwa wawakilishi wake.
NCHI TISHIO
Nchi ambazo ni tishio kwa Tanzania juu ya nafasi ya kuingiza timu nne msimu ujao ni Ivory Coast, Kenya, Msumbiji na Zimbabwe.
Mataifa hayo licha ya kuzikaribia pointi za Tanzania, pia baadhi yamefanikiwa kuingiza timu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku mengine yakiwa na uwezekano wa kuingiza timu kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
Ivory Coast ina pointi 15, timu yake ya San Pedro imetinga hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho na kama itapenya na kufanya vyema maana yake itavuka pointi za Tanzania ikiwa Yanga haitofuzu na kufanya vizuri.
Ni kama ilivyo kwa Kenya yenye pointi 14 ambayo inaweza kuziongeza na kuivuka Tanzania ikiwa timu zake mbili za Bandari na Gor Mahia zitatinga hatua ya makundi na kutamba.
Kuna Msumbiji yenye pointi 13 ambayo kuna uwezekano wa timu yake ya UD Songo kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika jambo linaloweza kuifanya iongeze pointi na pengine kuivuka Tanzania.
Tishio kubwa kwa Tanzania ni Zimbabwe ambayo licha ya kuwa na pointi nane, tayari timu yake ya FC Platinum imeshatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo alama ambazo timu hupata ni kubwa zaidi ya zile za kwenye Kombe la Shirikisho kulingana na nafasi itakayomaliza.
Kana kwamba haitoshi, pia wana timu ya Triangle ambayo imetinga hatua ya mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika na ikiingia makundi basi hali itakuwa tete zaidi kwa Tanzania.
Kama hali ikiwa hivyo ni wazi kwamba presha kwenye mashindano ya ndani itakuwa kubwa kwa timu tatu za Yanga, Simba na Azam katika kuwania kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.
Maana yake ili kukata tiketi hiyo, kila moja italazimika kuibuka bingwa wa Ligi Kuu au Kombe la FA vinginevyo, italazimika kusubiri hadi msimu wa 2021/2022.
WASIKIE WADAU
Aliyewahi kuwa Kocha wa Serengeti Boys na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo alisema licha ya wawakilishi wengine kufanya vibaya, lakini nchi imebahatika kubaki na Yanga na kikubwa kinachopaswa ni mikakati ya pamoja ili iweze kufanya vizuri na kufika hatua ya makundi.
“Kwa sasa hatuzungumzii ishu ya Yanga bali ni kama taifa kwa maana kufanya kwake vizuri ni faida kwa wote, kwani kama timu zote zingeishia njiani ilikuwa ishara mbaya kwenye soka letu, lakini kwa sasa tuna sehemu ya kuanzia, hivyo tutafanya kila liwezekanalo ili kuona inafika mbali,” alisema Mirambo.
Naye kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, Ally Mayay alisema kikubwa kitakachoibeba Yanga hatua inayofuata ni kuwa na mipango ya mapema kuliko kukaa kimya baada ya mchezo uliopita.
“Tatizo Yanga inaonekana haikujipanga vizuri hasa kwenye michezo yake ya nyumbani kwa maana kama wangejiandaa na kuweka mikakati mizuri, basi michezo yake ya nyumbani ingekuwa inafanya vizuri, lakini kwa harakaharaka linaonekana hilo halipo, ndio maana ilishindwa kuwa na matokeo mazuri,” alisema.
“Endapo Yanga atafanya vibaya, basi tusahau mwakani kuwa na wawakilishi wengi kama ilivyo mwaka huu, labda tuwaombee mabaya Kenya na Ivory Coast ambao wanatukaribia kwenye pointi nao wafanye vibaya,” aliongeza Mayay.
Kikosi cha Yanga kilichojaa wachezaji wapya kinahitaji kupambana kiwerevu ili kutengeneza kombinesheni za ushindi.