Yanga yamshusha mrithi wa Mayele Dar

MASHABIKI wa Yanga wanadai kitu pekee ambacho kimesalia kwenye kikosi cha ni kusajiliwa kwa mshambuliaji anayejua kufunga na hilo nalo limeisha baada ya mabosi wao kumshusha kimyakimya mshambuliaji Emmanuel Mahop kutoka Canon Yaoundé.

Unavyosoma taarifa hii tayari Mahop yupo nchini na anasubiri kusaini mkataba wa miaka miwili kuanza maisha mapya na Yanga akija kuchukua nafasi ya mfungaji bora Fiston Mayele anayeondoka zake.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba usajili huo una baraka zote kutoka kwa kocha wao mkuu Miguel Gamondi ambaye  tayari alikuwa ana faili zima la raia huyo wa Cameroon.

Gamondi alikuwa anahitaji mshambuliaji atakayekuja kufanya kazi moja tu ya kufunga kwenye kikosi chake baada ya kujiridhisha kwamba tayari ana kila staa wa maana katika maeneo mengine.

Yanga wameficha Mahop katikati ya jiji kwenye hoteli moja kubwa ambapo jana alitarajiwa kuanza mazungumzo ya mwisho kisha kusaini dili hilo na kwenda moja kwa moja Avic Town kujiunga na wenzake.

Mahop wakati wowote atatambulishwa akipewa jezi namba 9 lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa kuna mchezo maalum utatumika kumtambulisha Mcameroon huyo mwenye uwezo wa juu wa kufunga mabao ya vichwa na mashuti ya mbali.

Yanga inapiga hesabu za kucheza mchezo mmoja wa kirafiki wiki ijayo mwishoni ambao utakuwa maalum kumtambulisha mshambuliaji huyo sambamba na kiungo wao mshambuliaji mpya Pacome Zouzoua ambaye licha ya kutambulishwa kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi lakini hakucheza mechi hiyo dhidi ya Kaizer Chiefs.

Rekodi ya Mahop ndiyo iliyowashawishi mabosi wa Yanga kumaliza haraka dili hilo baada ya kufanikiwa kufunga jumla ya mabao 15 katika mechi 20 za ligi ya Cameroon huku pia akitoa pasi tatu za mabao.

Mshambuliaji huyo anakwenda kufunga usajili kwa wachezaji wa kigeni ambapo tayari Yanga ilibakiza mtu mmoja pekee kufikisha idadi ya wachezaji 12, ambao wanahitajika kikanuni.

Yanga kwenye dirisha hili imeshawasajili wachezaji 6 wa kigeni viungo Pacome, Maxi Nzengeli, Mahaltse Makudubela 'Skudu', mabeki Gift Fred na Kouassi Yao na sasa mshambuliaji Mahop ambao watakwenda kuungana na kipa Djigui Diarra, beki Lomalisa Mutambala, viungo Khalid Aucho, Stephane Aziz KI, Jesus Moloko, na  mshambuliaji Kennedy Musonda.