Yanga yakabidhiwa rekodi 7 ngumu

Amiss Tambwe (kushoto) na Thaban Kamusoko (kulia)
Muktasari:
YANGA imekuwa ikitambia rekodi zake za kutwaa mara nyingi ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ile ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame mara mbili nje ya ardhi ya Tanzania ikiwa timu pekee nchini, lakini sasa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeipa kibarua klabu hiyo kuthibitisha kuwa wao ni wakali kwelikweli au la.
YANGA imekuwa ikitambia rekodi zake za kutwaa mara nyingi ubingwa wa Ligi Kuu Bara na ile ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame mara mbili nje ya ardhi ya Tanzania ikiwa timu pekee nchini, lakini sasa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeipa kibarua klabu hiyo kuthibitisha kuwa wao ni wakali kwelikweli au la.
Caf katika ratiba ya mechi za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imeikabidhi Yanga mabingwa wa kihistoria wa michuano ya Afrika, Al Ahly ikiwa na rekodi saba ngumu na kama Jangwani watawang’oa Waarabu hao watajijengea heshima kubwa.
Yanga imetwaa mataji ya Ligi Kuu mara 25, ikiwa timu pekee iliyotwaa mara nyingi ikiwaacha mbali wapinzani wao wa jadi, Simba waliotwaa mara 18, lakini sasa kibarua walichopewa na CAF mbele ya Ah Ahly ya Misri itawapa jeuri zaidi Afrika.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, ilivunja mwiko wao wa miaka 32 mbele ya Waarabu kwa kuifunga Al Ahly kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam mwaka juzi na kubakia kidogo iwang’oe kama sio mikwaju ya penalti ya Said Bahanuzi na Mbuyu Twite kushindwa kutinga wavuni katika mchezo wa marudiano ugenini.
Hata hivyo klabu hiyo ina nafasi ya kulipa kisasi kwa Al Ahly yenye rekodi saba za kusisimua Afrika, ikiwa ya kwanza kwa ukongwe barani Afrika ikiwa imeasisiwa mwaka 1907.
REKODI ZILIVYO
Al Ahly inatesa kwa rekodi ya kuchukua taji la ubingwa wa Klabu Bingwa Afrika wakiweka rekodi ya kulitwaa mara nane, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2013 ambao Simba ndiyo walioshiriki ligi hiyo kwa mara ya mwisho ilipotolewa na Recreativo do Libolo ya Angola katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao 5-0.
Pia Al Ahly imetwaa Kombe la Shirikisho mara 5, ya mwisho ni mwaka juzi ilipoing’oa Yanga katika Ligi ya Mabingwa na kudondokea kwenye Kombe la Shirikisho na kwenda kutwaa.
Katika Super Cup inayokutanisha bingwa wa Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Al Ahly imevuruga ikitwaa mara sita ikiwa rekodi pia, huku Ligi ya nyumbani imetwaa mara 37, ikiwa ni zaidi ya umri alionao Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro, aliyezaliwa miaka 36 iliyopita.
Katika Kombe la FA, Al Ahly pia imetwaa mara 33 ikiwa pia ni rekodi, kitu ambacho vijana wa Jangwani wanapaswa kufanya kweli kwenye mechi zao mbili za nyumbani na ugenini ili kujenga heshima Afrika.
UWANJA NAO
Yanga hawana uwanja wa mechi, wanatumia ule wa Taifa unaochukua mashabiki 60,000 lakini Al Ahly wanautumia Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, ambao una uwezo wa kuchukua watu 74,100 lakini klabu hiyo iliwahi kuweka rekodi ya kuingiza mashabiki 120,000.
Baadhi ya nyota wa Yanga na hata benchi la ufundi la klabu hiyo kupitia kocha Hans Pluijm wamejinasibu kuwa, mwaka huu lazima kieleweke kwani wangependa kufika mbali kwenye michuano hiyo licha ya kutambua ugumu uliopo mbele yao.
Yanga itaikaribisha Al Ahly Aprili 9 kabla ya kuifuata wiki moja baadaye mjini Cairo, na kama Yanga itafuzu itatinga makundi na iking’oka itaangukia Kombe la Shirikisho.