Yanga yaizima Simba, yabeba Ngao

Muktasari:

KLABU ya Yanga imefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Simba bao 1-0 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.  

KLABU ya Yanga imefanikiwa kutwaa Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Simba bao 1-0 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.  

Bao la Fiston Mayele katika kipindi cha kwanza limetosha kuipatia Yanga ushindi baada ya kuondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria kwenye hatua ya awali.

Simba ilianza kipindi cha pili kwa kuishambulia Yanga baada ya Didier Gomes kufanya mabadiliko katika kipindi cha pili ya kumtoa kiungo Hassan Dilunga na kumuingiza nahodha John Bocco.

Chris Mugalu alikosa bao la wazi dakika ya 48, ya mchezo baada ya shuti lake kupaa langoni mwa Yanga.

Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Farid Musa aliyetoa pasi ya bao kwa Mayele kisha nafasi yake kuchukuliwa na Yacouba Sogne dakika ya 70, ya mchezo kabla ya kutoka Fiston Mayele na nafasi yake kuchukuliwa na Heritier Makambo.

Zikiwa zimesalia dakika 4, kabla ya mchezo kumalizika kiungo wa Simba Taddeo Lwanga alipata kadi nyekundu baada ya kumchezea madhambi kiungo wa Yanga Feisal Salum 'Fei Toto'.

Licha ya mabadiliko kwa Simba ya kumtoa Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin, Mohamed Hussein 'Tshabalala' na nafasi zao kuchukuliwa na Pape Sakho, Peter Banda na Israel Patrick Mwenda ila hayakuweza kubadili matokeo ya mchezo wa leo hadi dakika 90, zinamalizika.

Ushindi wa leo unaamsha ari na hamasa kwa mashabiki wa Yanga pamoja na benchi nzima la ufundi likiongozwa na Nasredine Nabi na msaidizi wake Mburundi Cedric Kaze baada ya presha kubwa iliyokuwa inamkabili.

Yanga imelipa kisasi kwa Simba baada ya kufungwa kwenye mchezo wao wa mwisho waliokutana kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), Julai 25 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Mkoani Kigoma.

Baada ya mchezo wa leo Simba na Yanga zitakutana tena kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara Disemba 11.