Yanga yaitesa St. Louis kipindi cha kwanza

Muktasari:

Mchezo umekuwa wa kasi ambapo kila upande ulijaribu kusaka bao la mapema ili kuongeza presha kwa wapinzani.

Shelisheli. Kiujumla kipindi cha kwanza kilibalansi kutokana na timu zote kushambuliana kwa zamu.
Mchezo umekuwa wa kasi ambapo kila upande ulijaribu kusaka bao la mapema ili kuongeza presha kwa wapinzani.
Wenyeji St. Louis walitumia zaidi mbinu ya kupiga mipira ya juu ambayo mara kwa mara ilionekana kuwapa tabu walinzi na viungo wa Yanga lakini hata hivyo walisimama imara na kuhakikisha haileti madhara golini kwa Youthe Rostand.
Yanga wenyewe walitumia pasi za chinichini hasa kupitia kwa walinzi wake wa pembeni Hassan Kessy na Gadiel Michael.
Ilionekana staili hiyo ya Yanga ina faida zaidi kwani waliweza kutengeneza idadi ya nafasi takribani tano ambazo zilizua kashikashi langoni mwa St. Loius.
Baada ya kosakosa kadhaa za huku na kule, Ibrahim Ajibu aliwainua vitini Watanzania wachache waliojitokeza uwanjani hapo baada ya kuifungia Yanga bao la kuongoza akiunganisha vyema krosi ya chini chini iliyopigwa kutokea upande wa kulia na Hassan Kessy.
Pamoja na kufunga bao hilo, Ajibu alikuwa mwiba kwa mabeki na viungo wa St. Louis ambao mara kwa mara walimchezea faulo ili kumpunguza spidi.