Yanga yaitaka Azam FC Zanzibar katika vita ya ubingwa
Muktasari:
- Ikimalizana na Fountain Gate tu, Yanga itakwenda jijini Mwanza kucheza mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la CRDB, ikikutana na Azam FC, mechi ikipangwa kupigwa Uwanja wa CCM Kirumba.
YANGA inaendelea kupiga safari za mbali kwenye mechi zake za ugenini lakini ikajiongezea umbali zaidi ikiirudisha Azam FC, kwenye uwanja mmoja ambao matajiri hao wa Chamazi wameumia zaidi timu hizo zinapokutana.
Mchezo ujao wa Yanga itakuwa ugenini Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha itakapokuwa mgeni wa Fountain Gate inayofundishwa na Fred Felix Minziro aliyewahi kuichezea Yanga nafasi ya beki wa kulia, ambaye ameibadilisha timu hiyo ikirudi kuanza kupata ushindi kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja.
Ikimalizana na Fountain Gate tu, Yanga itakwenda jijini Mwanza kucheza mchezo wa nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho la CRDB, ikikutana na Azam FC, mechi ikipangwa kupigwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Ikimaliza mchezo huo, Yanga itatakiwa tena kuwa mwenyeji kucheza na Azam lakini ikirudi kwenye mechi za ligi, sasa mabosi wa klabu hiyo wakafikiria mechi hiyo ipigwe hapohapo CCM Kirumba lakini ratiba hiyo imekataliwa.
Kilichozuia maombi hayo ya Yanga ni siku hiyo ambayo ilitakiwa kucheza na Azam Juni 24 kwenye uwanja huo, wenyeji Pamba Jiji nao inatakiwa kuutumia kucheza dhidi ya Mbeya City.
“Ukiangalia safari zimekuwa ndefu sana tukasema tufanye maamuzi ya mchezo wetu wa pili na Azam, baada ya ule wa Shirikisho nao tuucheze palepale Mwanza, lakini tulipowasiliana na wenye uwanja wakasema hapana tayari siku hiyo walishautoa uwanja kuwa chini ya Pamba.
“Baada ya hilo, sasa Yanga imeshawasilisha maombi ya kucheza mechi hiyo kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar, ikitaka kukutana na Azam kwenye uwanja huo,” kilisema chanzo.
Rekodi zinaonyesha, msimu huu Yanga imekutana na Azam mara mbili kisiwani humo na mechi ya kwanza ilikuwa ya fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 na Yanga ikashinda kwa mikwaju ya penalti 5-4, mechi ikipigwa uwanja wa Gombani, Pemba.
Yanga tena ikakutana na Azam FC kwenye wa nusu fainali ya Kombe la Muungano 2026, ikashinda tena kwa mabao 2-1, ikienda fainali ambayo ikapoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba. Kumbuka Azam ilipokuwa mwenyeji wa Yanga katika ligi mzunguko wa kwanza, timu hizo hazikufungana.
Tangu Ibenge atue nchini, Yanga ndio timu pekee ambayo hajawahi kuondoka na ushindi mbele yake ambapo ametoa sare moja, akipoteza mbili.
Mchezo huu unatabiriwa kutoa picha halisi ya nani anaweza kuwa bingwa wa ligi msimu huu, pia nafasi ya kwenda kubeba Kombe la Shirikisho la CRDB kwani mshindi anatinga fainali kucheza na Simba au Coastal Union.