Yanga yaibana mbavu Simba

Friday October 02 2020
yanga pic

KAMA ulikuwa unadhani sakata la Bernard Morrison ‘BM3’ na klabu yake ya zamani Yanga

limeisha pole, kwani mabosi wa Jangwani wamelianzisha upyaaa baada ya kubaini kuna madudu kwenye mkataba mpya wa mchezaji huyo na klabu yake ya Simba.

Yanga wameibuka na hoja hizo ikiwa zimepita siku 55 tangu Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumuidhinisha kiungo mshambuliaji huyo kuwa mchezaji huru akitokea Yanga,

Agosti 12, TFF kupitia Kamati yake ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ilitangaza Morrison aliibuka kidedea na kumtangaza kuwa mchezaji huru kwa kudai mkataba wake mpya wa Yanga ulikuwa na upungufu na kushindwa kuwa halali.

Hatua hiyo ilimfanya Morrison kuwa huru kisha baadaye kujiunga na watetezi wa Ligi Kuu Bara Simba na kuanza kuitumikia timu hiyo kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa jijini Arusha na kucheza mechi zote nne za Ligi Kuu kwa timu yake zilizowapa pointi 10 na mabao 10.

Klabu ya Yanga kupitia Makamu Mwenyekiti wake, Fredrick Mwakalebela jana jioni, walisema wamebaini upungufu mkubwa katika mkataba wa Morrison na Simba ukiwa na makosa kama yaliyodaiwa kufanywa na wao na kuifanya TFF na kamati yake kumuondoa Yanga kibabe kwa kisingizio cha kuwa mchezaji huru.

Advertisement

Mwakalebela alisema katika mkataba wa Morrison na Simba uliopelekwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) umesainiwa na upande mmoja wa mchezaji, huku kukiwa hakuna saini ya kiongozi yeyote wa Simba, wala ya shahidi ambaye huwa ni mwanasheria sambamba na saini ya mjumbe yeyote wa Shirikisho la Soka kuidhinisha uhalali wake na kushangaa kama mkataba ulikuwa na upungufu alipata wapi uhalali wa kupata leseni ya ligi ili aitumie Simba.

“Kwa dosari hizo ni wazi hakuna uhalali wa Morrison kuitumikia Simba, kwani hakukidhi vigezo vya kupata leseni kwa maana hiyo Simba imemtumia kimakosa na kikanuni inastahili kupoteza mechi zote walizomtumia ikiwamo ya Ngao ya Jamii na nne za Ligi Kuu. Pia Yanga tunaendelea kuamini Morrison ni mchezaji wetu kwa sababu ana mkataba nasi wa miaka miwili,” alisema Mwakalebela na kuongeza;

“Kwa kuwa tayari tulishawasilisha rufaa yetu FIFA kupitia Mahakama ya Usuluhishi ya Kimichezo ya Kimataifa (CAS) na kulipia kila kitu nao walishatujibu wamepokea na kutaka kuwasilisha vielelezo na kupata hili itatusaidia kuthibitisha kuwa TFF ilimuidhinisha Morrison isivyo halali.”

Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alipoulizwa na Mwanaspoti jana juu ya madai hayo, alisema hawezi kusema lolote kwa vile ndio kwanza anasikia kutoka kwa mwandishi na kwamba anasubiri kuona madai hayo ya Yanga ili awe na nafasi ya kujibu.

“Ni ngumu kusema lolote, kwani sijui chochote katika unaloniuliza, nasubiri kujua madai hayo ya Yanga juu ya Morrison,” alisema Try Again.

Wakati TFF ikitangaza uamuzi wa kesi hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, Elias Mwanjara alisema walibaini upungufu wa mkataba wa Yanga na mchezaji huyo na kuzua utata kwa vile kesi ya msingi ilihusu dai la Morrison kukana kuwa na mkataba mpya Jangwani.

Uongozi wa Yanga ulikuwa unadai una mkataba mpya na mchezaji huyo baada ya ule wa awali wa miezi sita, huku Morrison akiukana na Yanga kuamua kumjumuisha kwenye orodha ya wachezaji wake na kupeleka TFF, lakini jina lake likakatwa na kuorodheshwa Simba na kusababisha Yanga kukimbilia FIFA.

 

Advertisement