Yanga wanajiamini sana Aisee!

Muktasari:
Wanaamini kuwa wataifunga timu hiyo na kusonga mbele licha ya watu wengi kuikatia tamaa kutokana na rekodi ya wenyeji wao.
YANGA wanajiamini sana! Hawana hofu yoyote juu ya pambano lao la kesho Jumamosi la marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Etoile du Sahel huko Tunisia.
Wanaamini kuwa wataifunga timu hiyo na kusonga mbele licha ya watu wengi kuikatia tamaa kutokana na rekodi ya wenyeji wao.
Yanga ipo ugenini kukabiliana na Etoile ambao walitoka nao sare ya bao 1-1 ktika pambano la kwanza lililochezwa wiki mbili zilizopita jijini Dar es Salaa na kesho wanahitajika sare ya zaidi ya mabao mawili ili kusonga mbele, ingawa inaonekana ni kazi ngumu kuliko hata iliyofanya kutwaa taji la Ligi Kuu Bara mapema.
Hata hivyo Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Boniface Mkwasa na baadhi ya nyota wake, wametamba kabla ya kuondoka nchini kwamba wanaenda kupambana na muhimu ni kuomba Watanzania wawaombee dua njema na wao watawapa raha ugenini.
Mkwasa alisema kuwa wanajua mechi ya kesho itakuwa ngumu, lakini vijana wao wameandaliwa kuwaduwaza Waarabu nyumbani kwao na kuwatoa hofua Watanzania kuwa hakuna kitakachoharibika.
“Ni mechi ngumu kweli, lakini Yanga tuna vijana wenye vipaji na uwezo mkubwa kisoka na wapo tayari kupambana baada ya kuwapa maelekezo ya kitu gani cha kufanywa uwanjani Jumamosi,” alisema Mkwasa.
“Cha kufurahisha wachezaji waliokuwa majeruhi wamerejea tena uwanjani na tunahakika tutakufa na Etoile ili kufuta dhana kwamba Yanga haiziwezi timu za Afrika Kaskazini, tunaomba dua njema za Watanzania na sisi tutawalipa kwa kuwatoa Watunisia.”
Naye beki wa pembeni Oscar Joshua ‘OJ’ alisema, wao ni kama wanajeshi wanaenda kupigana kwa manufaa ya taifa na hivyo hakuna haja ya Watanzania kuikatisha tamaa Yanga kwani vijana wapo tayari kujitoa kufanikisha lengo la klabu kuweka rekodi Afrika.
“Tunataka kuweka rekodi na kuvunja mwiko, tuliwakosakosa Al Ahly mwaka uliopita, safari hii hatutaki tufanye makosa hayo, tunamuomba Mungu atuwezeshe na nyie tuombeeni,” alisema OJ ambaye mwili wake mkubwa ulikuwa msaada mkubwa katika mechi iliyopita baina ya timu hizo.
Kama Yanga itafanikiwa kuing’oa Etoile, itasubiri kujua inacheza na timu ipi kati ya nane zitakazotupwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kuwania nafasi ya kufuzu hatua ya makundi. Al Ahly ya Misri ndiyo bingwa mtetezi.