Yanga Unbeaten, wabeba Kombe

DAKIKA 90 za mchezo wa Yanga na Simba zilimalizika katika fainali ya Kombe la Mapinduzi huku kukiwa hakuna timu iliyotikisa lango la mpinzani wake, mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Amaan kisiwani hapa hivyo kulazimika bingwa kuamulikwa kwa mikwaju ya penalti.

Baada ya penati hizo Yanga ilitangwa bingwa wa mashindano hayo baada ya kushinda kwa penati 4-3 baada ya mechi hiyo kumalizika bila kufungana ndani ya dakika 90.

Penati za Yanga zilipigwa na Tuisila Kisinda,  Abdallah Shaibu 'Ninja', Zawadi Mauya na Said Ntazobonkiza wakati Tonombe Mukoko akikosa

Upande wa Simba waliopiga ni penati hizo na kufunga ni Francis Kahata, Chris Mugalu, Gadiel Michael wakati Meddie Kagere na Joash Onyango wakikosa.

Dakika ya sita tu tangu kuanza kwa mchezo huo Miraji Athuman wa Simba alikosa bao akiwa amepiga shuti kali lililogonga mwamba na kutoka nje huku dakika tatu baadaye Saidi Ntibanzonkiza akipiga mpira uliompata Michael Sarpong aliyepaisha juu ya goli.

Safu ya ushambuliaji ya  Yanga ilionekana kutokuwa makini katika umaliziaji kwani Sarpong aliinyima tena timu yake bao dakika ya 25 baada ya kupiga mpira uliookolewa na kipa wa Simba, Beno Kakolanya baada ya mabeki wake kupoteza umakini wa kulinda hatari hiyo.

Mwamuzi wa mchezo huo, Nassir Salum Siahi alitoa kadi za njano kwa wachezaji watatu wa timu hizo akianza na David Kameta 'Duchu' baada ya kucheza rafu dakika ya 28 wakati Haruna Niyonzima wa Yanga naye akipewa kadi dakika ya 32 kwa kumchezea rafu Yassin Mzamiru huku kadi ya mwisho ya kipindi cha kwanza ikienda kwa Kennedy Juma wa Simba aliyemchezea rafu Kisinda dakika ya 45.

Simba walikosa bao dakika ya 38 baada ya Kahata kupiga mpira wa kona uliompata Joash Onyango aliyepiga kichwa na kutoka nje kidogo ya goli huku Sarpong akipoteza tena bahati dakika ya 38 baada ya kupiga shuti nje akipokea pasi nzuri ya Kisinda.

Timu hizo zilikwenda mapumziko zikiwa hazijafungana huku kila kitu ikionyesha kuwa na kiu ya kutwaa ubingwa huo ambapo mara ya kwanza zilikutana kwenye fainali za mashindano hayo mwaka 2011 ambapo simba waliibuka na ushindi.

Makocha wote wawili walifanya mabadiliko kipindi cha pili ambapo Cedric Kaze wa Yanga aliwatoa Adeyun Salehe/Paul Godfrey, Sarpong/Waziri Junior wakati upande wa Simba kaimu kocha mkuu Seleman Matola aliwatoa Hassan Dilunga aliyapata maumivu ya misuli ya paja nafasi yake ilichukuliwa na Chris Mugali, Miraji Athuman alipumzishwa na kuingia Ibrahimu Ajibu.

Katika kipindi hicho cha pili Niyonzima alipiga shuti kali dakika ya 47 akipokea mpira wa krosi uliopigwa na Kisinda lakini lilidakwa na Kakolanya huku Saido akipiga mpira wa faulo dakika ya 54 baada ya Kisinda kuchezewa rafu hata hivyo shuti hilo lilitua mikokoni mwa Kakolanya.

Ajibu naye alipaisha mpira akipiga shuti lililopita juu ya lango la wapinzani wao ikiwa ni dakika ya 90 ya mchezo huo.

Beki wa Simba, Onyango raia wa Kenya aliobuka Mchezaji Bora wa mechi hiyo ambapo alizawadiwa Sh 1 milioni akifikisha idadi ya wachezaji bora watatu kwa mechi tofauti kutoka Simba akianza na Miraji pamoja na Kahata.

Miraji pia ndiye alikuwa kinara wa mabao katika mashindano hayo akifunga jumla ya mabao manne.

Yanga: Farouk Shikhalo, Kibwana Shomari, Adeyun Salehe, Said Makapu, Abdallah Shaibu, Mukoko Tonombe, Tuisila Kisinda, Zawadi Mauya, Michael Sarpong, Said Ntibanzonkiza na Haruna Niyonzima.

Simba: Beno Kakolanya, David Kameta, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Joash Onyango, Tadeo Lwanga, Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Francis Kahata na Miraji Athuman.

Tangu yaanzishwe
2007- Yanga
2008- Simba
2009- Miembeni
2010- Mtibwa Sugar
2011- Simba
2012- Azam Fc
2013- Azam FC
2014- KCC
2015- Simba
2016- URA
2017- Azam FC
2018 - Azam FC
2019- Azam FC
2020- Mtibwa Sugar
2021 - Yanga