Yanga: Sasa mtakoma ubishi

MWANDISHI WETU BENCHI la ufundi la Yanga limetangaza rasmi kwamba kipindi kigumu kimekwisha na sasa ni kupepea tu na wameiambia Azam kwamba; "Tutauana kesho hapo Taifa." Yanga, ambayo usajili wake unakadiriwa kupita sh.mil.200 ilipata ushindi wa kwanza katika mechi tano za Ligi Kuu Tanzania Bara ilizocheza tangu kuanza kwa msimu mpya ambao awali waligomea kuvaa jezi zenye doa jekundu kifuani mpaka wadhamini walipobadili na kufanya jeusi. Kocha Msaidizi wa Yanga na beki wa zamani wa timu hiyo, Fred Minziro aliiambia Mwanaspoti kuwa ;"Tulikuwa kwenye wakati mgumu sana lakini sasa kila kitu ni freshi, gundu limeondoka na tunaanza mambo sasa, kila mtu akili yake iko freshi kabisa. Hiyo mechi na Azam nakwambia tutauana mpira utakaopigwa hapo si mchezo." "Katika mechi zote tulizocheza tumecheza vizuri lakini tatizo ilikuwa kwenye umaliziaji, magoli yalikuwa hayaingii lakini sasa hivi tumeshafunga na tumepata ushindi wachezaji wanajiamini zaidi. "Hii ni dalili nzuri kwamba kuanzia sasa mambo ni mazuri na ushindi utakuwepo bila wasiwasi, tutapambana sisi ndio mabingwa watetezi bwana,"alisema kocha huyo na kusisitiza kuwa hana tofauti zozote na kocha wake Sam Timbe kama inavyozushwa na baadhi ya watu. Mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga ambaye alikuwepo Chamanzi kushuhudia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya African Lyon juzi Alhamisi alisema; "Sasa ndio tunaanza ligi na tutatoa onyo kwa wapinzani wote walioko mbele yetu." Kocha wa Azam, Sterwart Hall amesema ameisoma Yanga vilivyo katika mechi dhidi Lyon wala hana wasiwasi kwani anaelewa jinsi ya kuikabili ingawa amekiri ni mchezo mkali na wa kuvutia kama ilivyokuwa walipotoka suluhu na Simba. Kikosi cha Azam kesho Jumapili; Obren Cuckovic, Erasto Nyoni, Wazir Omar, Said Morad, Agrey Morris, Ibrahim Mwaipopo, Mrisho Ngassa, Jabir Aziz, John Bocco, Kipre Tchetche, Ramadhani Chombo. Yanga; Yaw Berko, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Chacha Marwa, Bakari Mbegu, Nurdin Bakari, Shamte Ally, Rashid Gumbo, Keneth Asamoah, Davies Mwape, Kiggi Makasi.