Yanga, Nugaz wapigwa faini Bodi ya Ligi

Muktasari:
Adhabu hizi zimetolewa baada ya kamati hiyo kukaa katika kikao chao kilichofanyika Novemba 20 kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi.
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu, imempiga faini ya Sh 500,000 (Laki Tano) Afisa Muhamasishaji wa Yanga, Juma K Nugaz kwa kosa la kufanya mahojiano na vyombo vya Habari ndani ya eneo la kuchezea na kusababisha kuchelewa kwa mahojiano ya kikanuni ya makocha na manahodha wa timu zote mbili.
Tukio hilo lilitokea katika mchezo wa Gwambina dhidi ya Yanga, adhabu hiyo imetolewa kwa uzingativu wa kanuni ya 15 (54) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za michezo.
Yanga pia imepigwa faini ya sh 500,000 (Laki Tano) kwa kosa la mashabiki wao kuwapiga mawe na chupa waamuzi wakati wakiwa wanaelekea kwenye vyumba vyao vyao vya kubadilishia nguo.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingati akanuni ya 15(54) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti wa klabu.
Kamati hiyo pia imemfungia michezo miwili kocha wa Mwadui, Khalid Adam kwa kosa la kukataa kufanya mahojiano na wanahabari mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Simba dhidi ya Mwadui ambao walifungwa 5-0.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 43:2 (2.13) ya Ligi Kuu kuhusu udhibiti kwa makocha.
Wakati huo huo klabu ya Kagera Sugar imetozwa faini ya sh 200,000 (Laki Mbili) kwa kosa la kuchelewa kuingia uwanjani walipokutana na Mtibwa Sugar.
Kagera ambao walikuwa wenyeji wa mchezo huo walifika uwanjani saa 6:51 mchana badala ya saa 6:30 mchana (Muda uliowekwa kikanuni).
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 15 (54) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.