Yanga Moro yaikalisha Simba

Morogoro. Aina na staili ya ushangiliaji inayoendelea kupata umaarufu ya mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele katika Ligi Kuu ya NBC imeibukia kwa mashabiki wa klabu hiyo wakishangilia ushindi dhidi ya wenzao wa Simba SC kuonyesha unyonge baada ya kupoteza michezo ya kuvuta kamba.

Akizungumza baada ya mchezo huo mjini hapa, Fatuma Shabaan (68) amesema wao wamepoteza michezo ya kuvuta kamba kwa upande wa wanawaume na wanawake dhidi ya wenzao wa Yanga SC.

Fatuma amesema wamekubali kuwa wanyonge kwa sababu wamepoteza michezo na kuwa wapinzani wao wakiwaachia wakitamba.

“Wenzetu (Mashabiki Yanga) wamewini kwa kutushinda katika michezo ya kuvuta kamba wanawake na wanaume lakini mwamuzi alionyesha hira hasa kwa upande wa wanawake na yoyote ya yote wazee tumefurahi na tunaomba tuandaliwe michezo ya marudiano tulipize kisasi na michezo kama hii kwetu inatuondolea upwe pia.”amesema Fatuma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Uchumi Baraza la Wazee Wilaya ya Morogoro, Salim Sige amesema ili kutengeneza furaha na kuwaondolea msongo wa mawazo kwa wazee kwani michezo imekuwa ikitoa nafasi nzuri ya kurejesha furaha.

“Michezo imekuwa eneo linalotoa furaha kwa rika zote na hawa wazee tukiwaandalia michezo kama hii ya kuvuta kamba, kucheza bao, karata, mbio fupi itawafanya waondokane na mawazo ya upweke,” amesema Salim.

Katibu wa Baraza la Wazee Kata ya Kingolwira, Scolastica Mluge (67) amesema jumla ya wazee 467 wameshiriki mazoezi na kupima magonjwa ya shinikizo la damu na kisukari, urefu na uzito huku waliokuwa na tatizo wakishauriwa kwenda hospitali.

“Idadi ya wazee wote kuanzia miaka 60 na kuendelea kata ya Kingolwira wameshiriki uzinduzi wa baraza la wazee kata hii na wamepata huduma ya kupimwa afya na madaktari wetu,” amesema Scolastica.