Yanga mbili zote visu

YALAAAH! Kiungo mpya wa Yanga,Geofrey Mwashiuya akisikilizia maumivu wakati akichukuliwa vipimo vya afya jana jijini Dar es Salaam. PICHA NA SAID KHAMIS
Muktasari:
- Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm, alisema kila nafasi katika kikosi chake sasa ina nyota wawili ama watatu wenye uwezo unaokaribiana jambo ambalo linamfanya kuwa na kikosi kipana pengine kuliko timu nyingine yoyote nchini huku Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji, akisisitiza kwamba safari hii ameamua kumwaga fedha kusajili na akili yake ipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika tu.
UKIIACHA Azam FC kwa klabu zilizofanya usajili mpaka sasa, Yanga ndiyo nyingine inayoweza kutengeneza vikosi viwili imara uwanjani na benchi kukabakiwa na chenji.
Kocha wa Yanga, Hans Van Pluijm, alisema kila nafasi katika kikosi chake sasa ina nyota wawili ama watatu wenye uwezo unaokaribiana jambo ambalo linamfanya kuwa na kikosi kipana pengine kuliko timu nyingine yoyote nchini huku Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji, akisisitiza kwamba safari hii ameamua kumwaga fedha kusajili na akili yake ipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika tu.
Bilionea huyo amesema kwamba anataka kuondoka Yanga kwa kuwaachia kitu cha kujivunia ambacho ni ufanisi kwenye michuano ya kimataifa msimu ujao ambao ni mwakani.
Msimu uliopita Pluijm alilalamika kuwa na kikosi kidogo ambacho kilimpa wakati mgumu katika baadhi ya mechi hasa pale baadhi ya nyota wake walipokuwa majeruhji ama kuwa na ratiba ngumu.
“Nina kikosi kipana sasa, kila nafasi ina wachezaji wawili ama watatu na wote wana viwango vya juu, sina wasiwasi hata pale nitakapokuwa na majeruhi kadhaa kwenye timu. Ushindani mkubwa upo kwa sasa katika timu, kila mmoja anataka kuthibitisha ni bora zaidi ya mwingine, hii inanipunguzia ugumu wa kazi,” alisema kocha huyo wa zamani wa Chelsea ya Ghana.
“Kuna ushindani mkubwa zaidi katika safu ya ushambuliaji, kama unavyofahamu napenda timu yangu ipate matokeo hivyo nafasi hiyo ni nyeti zaidi, wachezaji wa nafasi hizo pia wanakuwa kwenye hatari ya kuumia sana.”
Yanga, mbali ya kuwa na nyota wawili ama zaidi katika nafasi moja, pia ina nyota kadhaa ambao wanamudu kucheza nafasi zaidi ya mbili uwanjani.
Nyota hao ni Mbuyu Twite anayecheza beki ya kati, pembeni na kiungo, Deus Kaseke, Geofrey Mwashiuya na Simon Msuva wanaomudu kucheza winga zote mbili.
Malimi Busungu pia anamudu kucheza winga na straika wa kati jambo ambalo linampa Pluijm wigo mpana zaidi. Pluijm alisema wiki hii watacheza mechi mbili za kirafiki ambapo leo Jumanne watacheza na KMKM ya Zanzibar na Jumamosi watacheza na kombaini Jeshi ili kukipima kikosi chake.
“Tutacheza mechi mbili za kirafiki, tutacheza na KMKM Jumanne na Jumamosi tutacheza na kombaini ya Jeshi, mechi hizi zitanisaidia kujenga kikosi changu. Natumaini baada ya mechi hizi nitakuwa nimepata picha halisi ya kikosi changu cha kwanza,” alisema Pluijm
ATAJA SIFA ZA FIRST ELEVEN
“Mchezaji wa kikosi changu cha kwanza lazima awe fiti kweli kweli, awe na mawazo chanya na utulivu wa akili, awe pia mpambanaji na kufuata mafundisho yangu ipasavyo. Kikosi kitakuwa kinabadilika kutokana na uwezo wa wachezaji unaoonyeshwa katika mechi na mazoezi ya kila siku, hakuna atakayejihakikishia nafasi,” alisema Pluijm.
VIKOSI VIWILI
Yanga kwa sasa ina vikosi viwili hatari ambavyo havitofautiani sana ubora na Pluijm anaweza kuamua kupeleka kikosi chochote uwanjani na kupata matokeo. Vikosi hivyo ni.
Kikosi cha kwanza
Ally Mustapha ‘Barthez’
James Zuttah
Oscar Joshua
Nadir Haroub
‘Cannavaro’
Kelvin Yondani
Mbuyu Twite
Haruna Niyonzima
Salum Telela
Donald Ngoma
Amissi Tambwe
Simon Msuva
Kikosi cha pili
Deo Munishi
Juma Abdul
Mwinyi Haji
Joseph Mapembe
Pato Ngonyani
Said Makapu
Geofrey Mwashiuya
Andrey Coutinho
Kpah Sherman
Malimi Busungu
Deus Kaseke
Benchi
Benedict Tinocco
Amosi Abel
Edward Charles
Hussein Javu