Yanga kushusha kocha Mtunisia, mbwembwe zamponza Mfaransa

YANGA inamshusha nchini kesho Aprili 20 kocha Nasreddine Al-Nabi, ambaye ni bonge la sapraizi kwa wadau wa karibu wa klabu hiyo ambao walishajihakikishia kwamba Sebastian Migne ndiye kocha wao.

Yanga ilifanya uamuzi mgumu juzi wa kuachana na Migne ambaye awali walishakubaliana naey kila kitu, lakini walipomtumia mkataba wa kazi akaanza tena mbwembwe za kutaka benchi zima lipigwe chini aje na watu wake kwani amesikia maneno ya hapa na pale.

Lakini Yanga wakakomaa kwamba haiwezekani huku wakimtaka aanze kwanza kwa muda na hao atakaowakuta kwani wamesaini siku si nyingi. Alipoendelea kukomaa wakampiga chini wakamvutia waya Al Nabi aliyewagomea Simba kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati akiwa Al Merrikh, ambaye leo atatua Dar kusaini na kuanza kazi fasta.

Kocha huyo mwenye uzoefu na soka la Afrika, ndiye aliyechukua nafasi ya Didier Gomes ndani ya Al Merrikh, lakini akafurushwa saa chache baada ya sare ya 0-0 na Simba mjini Khartoum, akiwa ni raia wa Ubelgiji mwenye asili ya Tunisia.

Kocha huyo anakuja kuziba nafasi ya kocha Cedric Kaze aliyetimuliwa mwezi uliopita saa chache baada ya Yanga kulazimishwa sare ya 1-1 na Polisi Tanzania katika mechi kali iliyopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha siku chache tangu walazwe 2-1 na Coastal Union.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga, zinasema kuwa  mabosi wa GSM wanamshusha Al-Nabi na hatakuja pekee yake ila na wasaidizi wake watatu watakaokuja kumsaidia majukumu katika timu hiyo.

Inaelezwa kwamba Al-Nabi atakuja na Kocha Msaidizi wake wa kwanza, Mtaalam wa mazoezi ya viungo anayekuija kuchukua nafasi ya Mghana Edem Mortotsi ambaye ameshatimka nchini.

Mortotsi alikuja katika benchi la Kaze na Yanga lilimtaka abaki lakini jamaa akaamua kuondoka hatua ambayo mabosi wa Yanga wameona ni nafuu kwao na kuachana naye juu kwa juu.

Yanga pia imemtaka Al Nabi aje na mtaalam wa kuchambua mikanda ya video ya timu pinzani kikosi ambacho alitua nacho katika kikosi cha El Merreikh lakini apopata sare dhidi ya Simba tu akapoteza kazi.

Hata hivyo, Kocha Juma Mwambusi anayeiongoza Yanga katika mechi mbili akishinda moja na kutoa sare moja atabaki katika timu hiyo na kwamba Mtunisia huyo analetwa fasta ili kesho awepo uwanjani akiishuhudia timu yake ikipambana na Gwambina ya Mwanza

“Naona viongozi wenzetu wameamua kufanya sapraizi hiyo, ili kukamilisha kabisa hatua ya kuunda benchi kubwa na jipya la ufundi,” alisema mmoja wa mabosi wa Yanga ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na kuongeza;

“Kocha atatakiwa kuja kuangalia timu kisha kushauri maeneo ya kuboresha katika suala zima la usajili wa wachezaji tayari kwa msimu mpya na ndio maana wameamua kumleta sasa.”


AL NABI

Kocha huyo aliyezaliwa Januari Mosi, 1965, amezifundisha klabu mbalimbali ikiwamo Al Ahly Benghaz ya Libya aliyoinoa kati ya mwaka 2012-2013, Al Hilal aliyokaa nao kwa mwaka msimu mmoja wa 2013-2014 na kutwaa nao ubingwa wa Ligi Kuu ya Sudan na pia kuifikisha timu hiyo robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2014 kabla ya kutimkia Ismaily ya Misri aliyoinoa msimu wa 2015-2016 kuchukua nafasi ya Mido, kisha kwenda Italia na kuiona Pont Donnaz Hone Arnad iliyopo Ligi Daraja la Nne msimu uliopita kabla ya kupewa ajira Al Merrikh kuanzia Januari 28 mwaka huu kuchukua nafasi ya Gomes aliyepo Simba na kucheza mechi tatu tu za Ligi ya Mabingwa Afrika, akipoteza mbili dhidi ya As Vita na Al Ahly na kuambulia suluhu nyumbani dhidi ya wababe wa Kundi A, Simba na kufurushwa Machi 7, sambamba na wasaidizi wake.