Yanga ilivyomlaza njaa Kingwendu

Muktasari:

  • Mzunguko wa kwanza Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo ilipigwa na Yanga mabao 5-1 na wa pili bado Wanajangwani wakashinda mabao 2-1.

Mchekeshaji mkongwe nchini, Rashid Mwinshehe 'Kingwendu' ni Yanga lialia na kitendo cha timu hiyo kuifunga Simba ndani, nje msimu huu katika Ligi Kuu Bara kimemfanya asahau shida zake na kuupa moyo wake burudani, huku akisahau kula.

Mzunguko wa kwanza Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo ilipigwa na Yanga mabao 5-1 na wa pili bado Wanajangwani wakashinda mabao 2-1.

Moja ya vitu alivyovizungumza kwenye mahojiano yake na Mwanaspoti ni kuhusu  Kariakoo Dabi ya Aprili 20, baada ya Yanga kushinda alijikuta analala bila kula jinsi ambavyo alikuwa anajisikia furaha, kuona amepata kitu cha kutamba nacho mtaani.

"Baada ya Yanga kushinda usiku nilisahau kula hadi mke wangu akaniambia mume wangu umetengewa chakula mezani. Nikamwambia raha niliyonayo moyoni sijisikii njaa kabisa," amesema Kingwendu ambaye hakula.

"Yanga imesajili wachezaji ambao hawatupi presha, ukienda kuangalia mechi unakuwa na uhakika wa ushindi, hilo ni jambo linalotakiwa kuigwa na timu nyingine, ambazo zinapata nafasi ya kushindana kimataifa.

"Lakini mchezaji wangu pendwa kabisa alikuwa Fiston Mayele, niliumia baada ya staa huyo kuondoka, jamaa alikuwa na mbio, nguvu, alikuwa akiwepo uwanjani moyo unakuwa na amani, ninaloweza kuwaomba viongozi wa Yanga wasajili mtu wa aina yake kikosini."