Yanga ijipange hasa kwa Mokwena

Muktasari:
- Habari hii imetusisimua wengi hapa maskani maana Mokwena ni kocha mkubwa sana Afrika hivi sasa na wasifu wake unajieleza wala hakuna haja na sababu ya kubishana katika hilo.
TUMEONA na kusikia tetesi miongoni mwa makocha ambao Yanga inawapigia chapuo kurithi mikoba ya Miloud Hamdi ni aliyekuwa Kocha wa Wydad Casablanca, Rulani Mokwena.
Habari hii imetusisimua wengi hapa maskani maana Mokwena ni kocha mkubwa sana Afrika hivi sasa na wasifu wake unajieleza wala hakuna haja na sababu ya kubishana katika hilo.
Hauwezi kusema kocha ambaye amewahi kuchukua ubingwa wa mashindano ya African Football League ni kocha wa kawaida au mdogo kwa vile tu ameshindwa kutamba akiwa na Wydad.
Ni kocha ambaye timu nyingi Afrika zimekuwa zikitamani kuwa naye kwa vile ana vituvitu na anafundisha soka vizuri hivyo ambayo inafanikiwa kumchukua inakuwa imelamba dume.
Kwa maana hiyo, kama Yanga inamuwania Mokwena ni jambo la kheri lakini inapaswa kufahamu sio shughuli nyepesi kumshawishi kocha mkubwa kama huyo kuja hapa nchini kuifundisha.
Kwanza inapaswa kuandaa mzigo wa maana wa fedha kwa vile kocha huyo ni wa daraja la juu na katika miaka ya hivi karibuni amelipwa mishahara ya kiasi kikubwa cha fedha katika timu ambazo amezifundisha kwa maana ya Wydad na Mamelodi Sundowns.
Ndiyo anaweza kupunguza kiwango cha mshahara ili ajiunge na Yanga lakini siku zote iko wazi kukonda kwa ng'ombe hakumfanyi awe kama sungura.
Lakini kitu kingine ni iwapo itampata, Yanga itapaswa kuhakikisha inaishi maisha yatakayoendana na kocha huyo na siyo vinginevyo.
Mokwena ni kocha ambaye hapana shaka atahitaji bajeti kubwa katika ujenzi wa kikosi chake, fedha ambazo atazitumia kwa ajili ya kusajili wachezaji wakubwa na watakaoamua matokeo ya mechi zake.
Siku zote kizuri huwa gharama hivyo Mokwena anaweza kuja Tanzania lakini watakaomleta wanapaswa kujifunga mkanda kwelikweli.