Yanga, Baobab zawekwa kiporo

Muktasari:

  • Taarifa ya TFF imeeleza kuwa mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) utapangiwa tarehe nyingine na taarifa rasmi itatolewa ikiwa haijaeleza kwa kina changamoto gani iliyoikumba Baobab.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeahirisha mchezo kati ya Yanga Princess na Baobab Queens uliopangwa kuchezwa leo katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kutokana na kile kinachoitwa changamoto.

Taarifa ya TFF imeeleza kuwa mchezo huo wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) utapangiwa tarehe nyingine na taarifa rasmi itatolewa ikiwa haijaeleza kwa kina changamoto gani iliyoikumba Baobab.

"Shirikisho la mpira wa miguu linapenda kukujulisha kuwa mchezo namba 50 wa ligi kuu ya wanawake kati ya Yanga na Baobab umeahirishwa utapangwa tena na taarifa zitatolewa hii ni kutokana na Baobab kupata changamoto, TFF inakuomba kuzingatia mabadiliko," ilisema taarifa hiyo.

Katika mzunguko wa kwanza, Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 mchezo ambao ulichezwa mjini Dodoma.

Hii sio mara ya kwanza kwa mechi za ligi hiyo kuahirishwa katika siku ya mchezo, kwani JKT Queens iliwahi kugoma kucheza dhidi ya Simba Queens katika Uwanja wa Azam Complex ikidai mechi hiyo ilipaswa kupigwa katika dimba lake la Meja Jenerali Isamuhyo.

Hata hivyo, baadaye timu hiyo ilitozwa faini na kupokwa alama.