Yanga, Azam kupigwa usiku

Muktasari:

  • Yanga inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 57 wakati Azam iko nafasi ya tatu na pointi zake 50

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya mabadiliko ya muda wa mchezo wa Ligi Kuu baina ya Yanga na Azam, Aprili 25 kwa kusogeza mbele muda wa mechi kuanza kwa saa 2:15 kutoka muda uliokuwa umepangwa mwanzoni wa saa 1:00 usiku.

Taarifa iliyotolewa na TPLB leo imeeleza kuwa mabadiliko hayo ya muda wa kuanza kwa mechi yamefanyika kutokana na Uwanja wa Benjamin Mkapa ambao utatumika kwa mechi hiyo kuwa na matumizi mengine.

"Mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Na. 251 kati ya Yanga na Azam utachezwa saa 2:15 usiku Aprili 25, 2021 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa badala ya saa 1:00 usiku kama ilivyotangazwa hapo awali.

Sababu ya mabadiliko hayo ni uwanja huo kuwa na matumizi mengine mchana," ilifafanua taarifa hiyo ya TPLB.

Timu hizo zitakutana huku Azam FC ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 katika mechi ya kwanza ambayo walikuwa nyumbani Uwanja wa Azam Complex iliyochezwa Novemba 25, bao pekee la ushindi likipachikwa na Deus Kaseke.

Siku hiyo ya Aprili 25 ambayo Yanga na Azam FC zitaumana, pia kutakuwa na mechi nyingine mbili siku hiyo ambapo Ihefu wataialika Coastal Union na Prisons watacheza na Ruvu Shooting