Yanga akili mingi, wawaduwaza Waalgeria

Muktasari:

  • Kulikuwa na hofu Yanga ambayo ingekuwa faida kwa wenyeji kama mastaa muhimu wangekosa mechi hiyo ya kwanza muhimu kuisaka robofainali.

YANGA imetumia akili kubwa kuhakikisha kwamba wachezaji wao wote wanakuwepo kwenye ardhi ya Algeria siku moja kabla ya mechi na CR Belouizdad.  Usisahau pia kwamba Miguel Gamondi alishamaliza kusoma mchezo huo kwa kumtumia swahiba wake anayeishi Algeria.

Kulikuwa na hofu Yanga ambayo ingekuwa faida kwa wenyeji kama mastaa muhimu wangekosa mechi hiyo ya kwanza muhimu kuisaka robofainali.

Yanga, Ijumaa itakuwa na kibarua cha kwanza kucheza mchezo wa hatua ya makundi dhidi ya CR Belouizdad nchini Algeria utakaochezwa kuanzia saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Mabosi wa Yanga leo Jumanne alfajiri wameondoka na wachezaji wote ambao hawapo kwenye timu za Taifa ambao walifanya mazoezi Avic Town kwa lengo la kuwahi na kuwasubiri wachezaji wengine.

Rodgers Gumbo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga ameliambia Mwanaspoti kuwa: “Tumeandaa utaratibu mzuri ndani na nje ya Uwanja.”  

Alisema kwamba walijua ratiba hiyo na ndio maana wakatumia akili kuhakikisha kwamba kila mchezaji anafika Algeria kwa wakati na hata mawasiliano ni mazuri na timu za Taifa wakielewa umuhimu wa mchezo huo.

Wachezaji wengine wapo kwenye majukumu ya timu zao za Taifa na wanamaliza Novemba 21 kwa muda tofauti tofauti huku kipa Diara Djigui pekee yeye alimaliza jana Jumatatu akicheza dhidi ya Afrika ya Kati uwanja wa Stade du 26 Mars nchini Mali (saa 4:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki).

Kwenye Taifa Stars, Yanga ina wachezaji nane ambao ni Aboutwalb Mshery, Metacha Mnata, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Hamad, Nickson Kibabage, Mudathir Yahya na Clement Mzize.

Wachezaji hawa watakiwasha na Morocco leo usiku saa 4:00 kwenye Uwanja wa Mkapa ambayo inakadiriwa kuisha saa 5:45 usiku. Baada ya hapo ni safari ya kwenda Algeria na wamekatiwa tiketi kwenye Turkish Airlines itakayoondoka saa 10 alfajiri ya Novemba 22. Watakaa Uturuki kwa saa 1:50 kwa ajili ya kuunganisha hadi Algeria na watafika saa 10:15 jioni huku wakiwa wameondoka nchini alfajiri saa 10:20 na kuwa wamesafiri jumla ya masaa 13 na dakika 55.

Hivyo mastaa wa Stars watakuwa na siku moja tu ya kufanya mazoezi na wachezaji wenzao ambao watakuwa wameshafika Algeria.

Stephan Aziz Ki (Burkina Faso) na Khalid Aucho( Uganda) ambao wapo nchini Morocco wao watasubiriana na kusafiri usiku wa saa 8:35 na kufika Tunisia saa 5:00 asubuhi kisha watapumzika masaa mawili na saa 6:20 mchana wataanza safari ya kwenda Algeria na watafika saa 7:40 mchana.

Azizi Ki yupo kwenye timu ya Taifa ya Burkina Fasso itacheza mchezo wake dhidi ya Ethiopia saa 4:00 usiku huku Uganda ya Aucho ikicheza na Somalia saa 10:00 jioni.

Upande wa Djigui yeye alicheza jana usiku hivyo ni wazi atapata muda wa kupumzika, anaweza akatoka na ndege ya Uturuki saa 7:50 usiku akafika Uturuki saa 11:20  asubuhi kisha atapumzika masaa matatu na saa 8:0 ataanza safari ya kwenda Algeria ambako atafika saa 10:15 jioni.

Wakati mastaa wa Yanga wakiwa wanahaha kusafiri usiku kucha, wapinzani wao CR Belouizdad yenyewe haina mchezaji wao yoyote yule timu ya Taifa ya Algeria jambo ambalo ni faida kwao na walinukuliwa kwenye mitandao yao ya kijamii wakifurahia changamoto za Yanga.

Belouizdad pia mechi yao ya mwisho kucheza ni jana Jumapili ikicheza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya JS Kabylie na kushinda bao moja lililofungwa dakika ya 90+ na Mouad Hadded.

Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kikosi chao kitasafiri kwa makundi huku akikiri ugumu wa ratiba kwao lakini hawana budi kukabiliana nao. Endelea kufuatilia mitandao yetu ya kijamii kwa habari zote za mechi hii.