Yakoub afanyiwa upasuaji, atakosekana hadi nusu ya msimu ujao
Muktasari:
- Kipa huyo amekuwa nje ya kikosi kwa karibu msimu mzima kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Morocco, hatimaye amekubali kufanyiwa upasuaji baada ya awali kusita kuchukua hatua hiyo akiamini angeweza kupona kwa matibabu ya kawaida.
SIMBA imepata pigo jingine baada ya kipa wake, Yakoub Suleiman kufanyiwa upasuaji wa goti lake utakomuweka nje ya uwanja hadi nusu ya msimu ujao.
Kipa huyo amekuwa nje ya kikosi kwa karibu msimu mzima kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa kwenye mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Morocco, hatimaye amekubali kufanyiwa upasuaji baada ya awali kusita kuchukua hatua hiyo akiamini angeweza kupona kwa matibabu ya kawaida.
Yacoub ambaye alitua Simba msimu huu akitokea JKT Tanzania, alikuwa kama mbadala wa Moussa Camara ambaye naye alipata majeraha akiwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa, lakini hesabu hizo ziligonga mwamba baada ya Mzanzibari huyo kukumbwa na janga pia.
Mzanzibar huyo aliyewahi kuchezea kikosi cha JKU, tangu atue Simba amefanikiwa kucheza mechi nne pekee za ligi, huku mchezo wa mwisho ni ule dhidi ya Azam Desemba 12,2025 ambako wekundu walichezea kipigo cha mabao 0-2 uwanja wa nyumbani na kimataifa amecheza mechi mbili tu.
Kukaa nje kwa Yacoub ambaye bado anamkataba wa miaka miwili ndiko kulikompa ulaji kipa Mahamadou Djibrila Kassali, ambaye alitua Simba dirisha dogo ingawa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zilisema kuwa upasuaji huo umefanyika kwa mafanikio na sasa mchezaji huyo ameanza programu maalumu ya kuuguza jeraha lake chini ya usimamizi wa madaktari, huku akitarajiwa kurejea uwanjani baada ya kukamilisha hatua zote za matibabu na mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili.
“Yakoub kwa muda mrefu alikuwa anasita kufanyiwa upa suaji, naw eza kusema hakuwa amepona alikuwa bado ana tatizo lilelile,”alisema bosi huyo wa Simba
“Baada ya kumuelewesha kwa muda mrefu hatimaye hivi karibuni akakubali maana aliona kabisa alikuwa anapata nafuu tu lakini sio kupona na amefanyiwa upasuaji wa goti lake ataanza hatua mpya ya kupona sawasawa.
“Msimu huu hawezi kabisa na hata msimu ujao atakuwa nje kwa nusu msimu itategemea na hatua ya uponaji wake, kama angekuwa wakati ule amekubali msimu huu angeweza kuwa tayari huku mwishoni au msimu ujao angeanza.”
Akizungumzia hilo Msemaji wa Simba, Ahmed Ally, amekiri kuwa kipa huyo amefanyiwa upasuaji huku akiomba kusubiriwa kwa ripoti kamili ya madaktari kujua muda ambao atakuwa nje.
“Ni kweli Yakoub amefanyiwa upasuaji, umefanyika hapa hapa nchini, ni hatua muhimu kwake ili aweze kupona sawasawa,bado sijajua atakuwa nje kwa muda gani, lakini tutatoa taarifa kamili baada ya kupata ripoti kamili,”alisema Ahmed
Kuendelea kukosekana kwa Yakoub hadi msimu ujao, kunaweza kuwa fursa kwa Kassali ambaye ameonyesha kiwango bora akiwa amecheza mechi 17 za ligi akiwa na cleansheet 12.
Kipa huyo wa timu ya taifa ya Niger rekodi zake ni bora kwani katika mechi tisa za mwanzoni aliruhusu jumla ya mabao matano tu.