Dar Leopards waliamsha Raga Dar
Muktasari:
- Mashindano hayo yamekuwa yakivuta mamia ya washiriki na watazamaji kila mwaka, yanatarajiwa kukutanisha timu 20 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki katika siku nzima ya michezo, burudani na shughuli za kijamii zinazolenga kuendeleza mchezo wa raga nchini.
WAPENZI wa mchezo wa raga jijini Dar es Salaam wanatarajia kushuhudia wikiendi yenye shamrashamra na ushindani mkubwa baada ya klabu ya Dar Leopards RFC kwa kushirikiana na wadhamini wake wakuu Roadgrip kurejea kwa mashindano ya kila mwaka ya Touch Rugby yatakayofanyika Juni 13 kwenye Uwanja wa Ufundi, Mikocheni.
Mashindano hayo yamekuwa yakivuta mamia ya washiriki na watazamaji kila mwaka, yanatarajiwa kukutanisha timu 20 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika Mashariki katika siku nzima ya michezo, burudani na shughuli za kijamii zinazolenga kuendeleza mchezo wa raga nchini.
Lengo la mashindano hayo ni kuendelea kuhamasisha ushiriki wa mchezo wa raga kwa watu wa rika zote, huku yakitoa nafasi kwa wachezaji wenye uzoefu na wale wanaoanza kujifunza mchezo huo kushiriki katika mazingira rafiki na yenye ushindani wa kiafya.
Katika toleo la mwaka huu, mabingwa watetezi Karen Crusaders wanatarajiwa kurejea dimbani kutetea ubingwa wao dhidi ya timu zitakazotoka Dar es Salaam, Zanzibar, Nairobi, Iringa na Arusha ambazo tayari zimeonyesha dhamira ya kufanya vizuri kwenye tamasha hilo.
Mbali na michezo ya uwanjani, waandaaji wameandaa burudani mbalimbali zitakazowafanya watazamaji kufurahia siku nzima. Kutakuwa na muziki, maeneo maalumu ya watoto, huduma za vyakula na vinywaji pamoja na mazingira rafiki kwa familia yatakayoruhusu kila mtu kushiriki bila malipo yoyote ya kiingilio.
Akizungumza na Mwanaspoti kuelekea mashindano hayo, uongozi wa Dar Leopards RFC ulieleza kuwa tukio hilo limekuwa zaidi ya mashindano ya michezo kwani limegeuka kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha jamii ya raga na kukuza urafiki miongoni mwa washiriki.
“Touch Rugby Tournament si mashindano pekee, bali ni sherehe ya michezo, urafiki na mshikamano wa jamii. Kila mwaka tunaona familia ya raga ikizidi kukua na tunawashukuru wadhamini pamoja na wadau wote wanaoendelea kutuunga mkono ili kufanya tukio hili kuwa kubwa zaidi,” ilieleza klabu hiyo.
Mashindano hayo yataanza saa 3:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni katika Uwanja wa Ufundi, huku waandaaji wakitoa mwaliko kwa wapenda michezo, familia, kampuni mbalimbali na wananchi kwa ujumla kujitokeza kushuhudia siku ya kipekee ya raga, burudani na mshikamano wa kijamii.