Prime
Winga mpya Yanga apewa miwili

Muktasari:
- Nyota huyo mpya kutoka DR Congo aliyekuwa nchini tangu wiki iliyopita wakati wa pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na TP Mazembe, anatokea AS Vita akimchomoa Jean Baleke aliyeonyeshwa mlango wa kutokea kutokana na kutokuwa katika mipango ya kocha Sead Ramovic.
YANGA ipo Mauritania ambapo kuanzia saa 4:00 usiku leo Jumapili itashuka uwanjani kumalizana na Al Hilal ya Sudan katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mapema mabosi wa klabu hiyo wameamua kufanya kweli kwa kumpa mkataba wa miaka miwili mshambuliaji mpya anayemudu winga zote, Jonathan Ikanga Lombo.
Nyota huyo mpya kutoka DR Congo aliyekuwa nchini tangu wiki iliyopita wakati wa pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na TP Mazembe, anatokea AS Vita akimchomoa Jean Baleke aliyeonyeshwa mlango wa kutokea kutokana na kutokuwa katika mipango ya kocha Sead Ramovic.
Habari kutoka ndani ya Yanga zinaeleza kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 amepewa mkataba huo baada ya Ramovic kumkubali, ingawa suala la kuanza kutumika linategemea na mabosi wa klabu hiyo wakimalizana na Fifa juu ya adhabu iliyotokana na kesi iliyofunguliwa na Mghana Augustine Okrah.
"Jonathan tayari amepewa miaka miwili baada ya kocha kuridhia asajiliwe na kilichobaki sasa ni kuanza kucheza kama ilivyo kwa Israel Mwenda mara baada ya Okrah kupewa chache na kuiondolea klabu adhabu ya kutosajili iliyopo kwa sasa kutoka Fifa," kilisema chanzo hicho.
Mapema mara baada ya Mwanaspoti kutoa taarifa juu ya kuwepo kwa mipango ya kusajiliwa kwa Jonathan aliyekuwa kocha wa AS Vita aliyewahi pia kuifundisha Yanga, Raoul Shungu aliweka bayana kwamba Yanga ikimsajili nyota huyo italamba dume kwani ni mchezaji atakayeipa mengi uwanjani.
Taarifa zaidi kutoka Yanga zinaeleza kuwa baada ya Jonathan kumalizana na klabu hiyo ili kuanza kuitumikia kinachoendelea kwa sasa ni makubaliano baina ya Yanga na Vita kuhusu kulipana ada ya uhamisho kabla ya kutumiwa ITC yake ili mambo yasiwe mengi kwa mchezaji huyo.
Ujio wa Jonathan ulikuwa ukizua swali kwamba atachukua nafasi ya mchezaji gani kwani Yanga ilikuwa imeshakamilisha wachezaji 12 wa kigeni, lakini imebainika anachukua nafasi ya Baleke ambaye imeamua kuachana naye.
Baleke alisajiliwa kupitia dirisha kubwa lililopita na kuifungia Yanga bao moja katika Ligi Kuu, lakini hakupewa muda wa kutosha kuitumikia chini ya makocha wote kuanzia Miguel Gamondi aliyeondolewa na Ramovic, na alikuwa apelekwe kwa mkopo Namungo, lakini mwenyewe ametaka kuvunjiwa mkataba aondoke zake.
Nyota huyo wa zamani wa Simba alisajiliwa na Yanga kutoka Libya alikokuwa akiichezea kwa mkopo kutoka TP Mazembe iliyo na mkataba naye, tangu alipotua nchini na kuitumikia Wekundu wa Msimbazi.