Winga Mghana bado kidogo tu Simba

WINGA Mghana Agustine Okrah huenda akawa mchezaji wa kwanza kunaswa kati ya wale wanne wanaonyatiwa na Simba baada ya kocha mkuu wa timu anayoichezea kwa sasa Bechem United, Kassim Mingle kuweka wazi uwezekano wa nyota huyo kukipiga kwa msimu ujao.
Kocha huyo amethibitisha kuwepo kwa dili baina yao na Simba sambamba na timu nyingine ambazo zinamtaka, lakini kwa ukubwa wa Wekundu hao anaamini huenda huko kukamfaa zaidi.
"Okrah ni mchezaji mzoefu, kama kuna fursa za kutoka nje ya nchi zitajitokeza basi hatutamzuia kwani ana muda mchache wa kucheza, Hatutamuuza timu yoyote ya hapa (Ghana), tunadhani ni vyema akaenda nje na zipo zinazomhitaji ikiwamo Simba. Anaweza kuwa faida kwetu kwa msimu ujao," amesea Mingle aliyewahi kuicheza Asante Kotoko ya nchini humu.
Okrah mwenyewe hivi karibuni alinukuliwan na kituo kimoja cha redio cha nchini, akiweka ahadi ya kuhakikisha timu yake inachukua Kombe la FA.
"Kwa sasa nafikiria zaidi kumaliza nafasi ya tatu kwenye ligi sio mbaya, ila sasa akili zetu pamoja nguvu tumeziwekeza kwenye mchezo wa fainali ya FA naamini tutashinda," alisema Okrah.
Simba inaendelea kusaka wachezaji wa kuimarisha kikosi chao kwa msimu ujao, baada ya kupoteza Ngao ya Jamii na Kombe la Ligi Kuu Bara kwa Yanga na ishalitema Kombe la ASFC linalowaniwa na Yanga na Coastal Union zitakazopetana kwenye fainali Julai 2, jijini Arusha.