Waziri Mkuu Bulgaria amtaka rais FA kujiuzulu kwa ubaguzi nyota wa England

Muktasari:

Wachezaji weusi wa England walifanyiwa vitendo vya ubaguzi wa rangi na mashabiki wa Bulgaria katika mchezo baina ya nchi hizo.

Sofia, Bulgaria.Waziri Mkuu wa Bulgaria, Boyko Borisov amesema serikali yake imesitisha mahusiano yote pamoja na kutoa fedha kwa Shirikisho la Soka la Bulgaria hadi pale rais wa FA, Borislav Mihaylov atakapojiuzuru.

Kiongozi huyo wa FA, Mihaylov ambaye pia ni mjumbe wa mkutano mkuu wa UEFA, ameitumia siku ya Jumatatu kabla ya mchezo wa Euro 2020 akidai wachezaji wa England pamoja na Tammy Abraham wangepata upinzani mkali pamoja ubaguzi jijini Sofia. Pia alisema mashabiki watukutu wa Bulgaria kufanya vitendo vya ubaguzi si jambo sahihi.

Mechi ililazimika kusimama mara mbili jijini Sofia kutokana na vitendo vya ubaguzi katika mchezo huo ambao England ilifanikiwa kushinda mabao 6-0.

England ilicheza katika mazingira magumu baada ya mashabiki wa Bulgaria kuwafanyia vitendo vya ubaguzi wachezaji wenye asili ya Afrika.

Raheem Sterling aliyefunga mabao mawili aliandamwa sana na mashabiki hao waliokuwa wakimuita nyani. Mabao mengine yalifungwa na Marcus Rashford, Ross Barkley (mawili) na Harry Kane.

Mchezo ulilazimika kusimama mara mbili baada ya wachezaji wa England kumvaa mwamuzi wakipinga vitendo vya mashabiki hao.

Kocha wa England Gareth Southgate aliwatuliza wachezaji wake na mara kadhaa alikwenda kulalamika kwa mwamuzi kuhusu matukio hayo.

Mchezo huo ulisimama dakika ya 43 baada ya Southgate kutoa malalamiko kwa mwamuzi kabla ya kuendelea. Awali ulisimama dakika ya 28.

“Niliona kundi la watu wapatao 50 wakiwa wamevaa mavazi ya rangi nyeusi wakitoa ishara mbaya ikiwemo saluti yenye mrengo na masuala ya kiasa,”alisema Mwenyekiti wa Chama cha Soka Greg Clarke.

Ufaransa ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Uturuki, Kosovo iliilaza Montenegro mabao 2-0, Lithunia ilicharazwa 2-1 ilipovaana na Serbia, Iceland ilichapwa 2-0 dhidi ya Andora na Albania ilishinda 4-0 ilipomenyana na Moldova.