Waziri Jr ataka kiatu Kagame

STRAIKA Wazir Junior wa Yanga amesema kombe la Kagame itakuwa ni sehemu yak ya kipimo cha kuhakikisha anakuwa mfungaji bora baada ya kuanza na bao moja kwenye sare 1-1 dhidi ya Big Bullets.

Junior na wachezaji wenzake wa timu kubwa wamebakizwa katika timu hiyo kwa lengo la kupata muda mwingi wa kucheza baada ya kutopata muda mwingi kwenye Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Junior alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha anachukua kiatu cha ufungaji bora kwenye kombe la Kagame licha ya changamoto kubwa ya kikosi inayoonekana kwenye timu yao.

Junior alisema timu nyingi kwenye kombe hilo wameingia na wachezaji wao kamili, upande wa timu yao umechanganya wachezaji wa timu kubwa wachache na wa timu ndogo wengi hivyo anabidi apambane kuweza kutimiza lengo lake.

"Yanga kwa asilimia kubwa ya wachezaji wamepumzika, hapa tumechanganyika kwahiyo kuna ugumu utakaokuwepo ila tutapambana kuhakikisha timu inafanya vizuri, upande wangu pia kutimiza malengo yangu," alisema Junior.

Junior katika Ligi amemaliza akiwa na mabao mawili licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara, upande wa Kagame Cup ameanza kwa kufungua akaunti ya mabao.