Watatu waziba pengo la Opah

Muktasari:

  • Opah ametimkia klabu ya Beskitas kucheza soka la kulipwa kutoka Simba

OPAH Clement ameanza kuyazoea maisha mapya nchini Uturuki, huku timu aliyokuwa akiichezea, Simba Queens imewataja wachezaji watatu wa kuziba nafasi yake kikosini.

Opah ametimkia klabu ya Beskitas kucheza soka la kulipwa kutoka Simba na Kocha Mkuu wa Wekundu hao, Charles Lukula amesema anawatumia Asha Rashid 'Mwalala', Gentrix Shikangwa na Zainabu Mohamed 'Dudu' ili kumsahau mshambuliaji huyo aliyeondoka na mabao tisa katika Ligi Kuu.
Lukula aliyasema hayo juzi baada ya timu hiyo kushinda mabao 7-0 dhidi ya Tigers Queens ya Arusha na kufafanua amempa mechi tano Mwalala ili kujiweka sawa zaidi baada ya kukaa nje kwa takribani miaka miwili na nusu.

Mabao ya mechi hiyo yaliwekwa kimiani na Shikangwa, Danai Bhobho, Joelle Bukuru, Olaiya Barakat, Amina Ramadhan na Asha Djafar aliyefunga mawili.

Kocha huyo alitaja sababu za kutowaingiza baadhi ya wachezaji wanaonekana kuwa bora zaidi kutokana na kutumika zaidi kwenye mechi nyingine kwa kuwapa mapumziko ili kujiandaa na mechi ijayo ya Derby Machi 23.

"Huu ni mpango wangu kuwaweka benchi Vaileth, Daniela, Corazone na Mnuka ili niwape mapumziko kidogo kwani mechi nyingi wamecheza na kuna mechi ngumu ya Derby  nitawatumia nina amini watanisaidia sana," alisema Lukula.

Ushindi wa juzi umeifanya Simba izidi kujikita kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi 26 na mabao 37, ikifuatiwa na Fountain Princess yenye pointi 23 na JKT Queens inafuata na alama 22 baada ya kila oja kucheza mechi 11.