Prime
Wataalamu wafunguka wimbi la majeraha Simba
MASTAA wa Simba wamekuwa wakipitia changamoto ya majeraha katika vipindi tofauti huku ikiwapoteza makipa watano ndani ya misimu miwili jambo ambalo limeonekana tishio kwa sasa.
Simba imepitia kwenye wakati mgumu kwa nyakati za hivi karibuni kutokana na mastaa wa timu hiyo wengi kupata majeraha ambayo yamekuwa yakiwaweka nje kwa vipindi virefu.
Awali aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Aishi Manula alianza kuumia goti mwaka 2023 na baada ya kwenda kwenye maandalizi ya msimu klabu hiyo iliziba pengo lake kwa kumsajili kipa kutoka Brazil, Jefferson Luis, ambaye pia aliumia akiwa kwenye mazoezi ya msimu na timu hiyo ilipoweka kambi Uturuki.
Baada ya madaktari kujiridhisha Luis atakaa nje kwa muda mrefu, aliachwa na timu hiyo ikaingia sokoni kumsajili Ayoub Lakred ambaye pia katikati ya msimu aliumia ndipo akasajiliwa Moussa Camara aliyejiunga na timu hiyo Agosti 2024 ili kuziba pengo lake na msimu wake wa kwanza 2024-2025 alimaliza kinara wa cleansheets 19 katika Ligi Kuu Bara, hata hivyo, kipa huyo aliongezewa mkataba uliotakiwa kumalizika Juni 30, 2026 lakini akaumia mwanzoni mwa msimu huu na kuelezwa atakaa nje kwa muda mrefu.
Baada ya Camara kuumia na kufanyiwa upasuaji wa goti la kulia, alitakiwa kukaa nje zaidi ya wiki 10 ili kuuguza majeraha yake, tegemeo la viongozi wa Simba lilikuwa kwa kipa mzawa, Yakoub Suleiman aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu akitokea JKT Tanzania alikomaliza msimu uliopita na cleansheets nane.
Hata hivyo, kipa huyo hakudumu kwenye ubora wake baada ya kupata majeraha ya goti akiwa na timu ya Taifa, Taifa Stars ikiwa inajiandaa mechi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) dhidi ya Nigeria, nchini Morocco yeye alikaa nje wiki mbili na sasa karejea kikosini.
Simba ilimuondoa Camara katika mfumo wa usajili wakati anaendelea kuuguza majeraha, ikamsajili mbadala wake, Djibrila Kassali ambaye ni kipa namba moja wa timu ya taifa ya Niger mwenye miaka 29.
Mbali na makipa, wachezaji wengine majeruhi Simba ni mabeki wa kati, Wilson Nangu na Abdulrazak Hamza ambao wanatakiwa kukaa nje hadi mwisho wa msimu kwa mujibu wa chanzo cha ndani ndipo watakapokuwa sawa kiafya.
Kwa upande wa kiungo mshambuliaji, Mohamed Bajaber aliyeumia tena dhidi ya Mtibwa Sugar, Januari 20, 2026, Uwanja wa Meja Generali Isamuhyo jijini Dar, mechi ikimalizika kwa sare ya bao 1-1, kabla ya hapo baada ya kutoka kusajiliwa tu mchezaji huyo aliumia na kukaa nje kwa muda mrefu.
Baada ya kupona alicheza mechi dhidi ya Mbeya City aliingia kuchukua nafasi ya Elie Mpanzu, katika ushindi wa mabao 3-0 walioupata Wanamsimbazi katika mechi hiyo alifunga bao mojawapo akipokea pasi ya mwisho ya Steven Mukwala huku kwa upande wa Bajaber taarifa zinasema ameanza mazoezi madogo madogo, lakini ikielezwa Simba imeshamwondoa kwenye mfumo wa usajili ili kuendana na idadi ya wachezaji 12 wa kigeni.
Baada ya matukio hayo, Mwanaspoti limewatafuta madaktari wa michezo, ambao kila mmoja ameeleza mtazamo wake kuhusu hali hiyo, huku wengine wakisema majeraha ya goti ni hatari zaidi kwa wanasoka duniani kwa kuwa yanachangia wachezaji kukaa nje muda mrefu.
Daktari mzoefu wa michezo, Shita Samwel ambaye anaandika Kolamu ya Spoti Dokta katika gazeti la Mwanaspoti kila Alhamisi, alisema jeraha linalochangia wachezaji kukaa nje kwa muda mrefu ni la goti (kukatika kwa nyuzi ligament iliyopo katikati, kama ikikatika daraja la tatu), kuchanika kwa misuli wa nyuma ya paja (daraja la tatu), kifundo cha mguu (inapohusishwa tishu laini kukatika pamoja na mvunjiko ya vijifupa) na mchezaji anapokuwa na mvunjiko.
"Sababu zingine kwa ujumla ni kucheza huku hajapona vizuri, umri mkubwa, mahala eneo la jeraha lilipo, matumizi holela ya dawa za maumivu, kujeruhiwa mara kwa mara, mchezaji kutumika sana bila kupumzika, mwili wa mchezaji kama kinga dhaifu, lishe duni, kutokupumzika, vilevile aina ya mazoezi kama hawazingatii utaalamu /waledi," anasema Shitta na kuongeza;
"Mara nyingi wachezaji viungo wa kati, mabeki wa kati ndio ambao wanakutana sana na majeraha kama unavyoona hapo, eneo hilo linaharakati nyingi wakati wa mchezo, soka inahusisha kukaba, faulo zinakuwa nyingi zaidi ukilinganisha na nafasi zingine,wanakumbana zaidi kimwili, hivyo kuna kukwatuliwa, kugongwa, kukatwa kwanja, siwezi kujua tatizo la hao wa Simba moja kwa moja, lakini unaweza kutazama mambo hayo niliyosema mojawapo linaweza kuwa limechangia."
Daktari wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', Gilbert Kigadye, alisema ingawa asilimia kubwa wachezaji wengi wanaumia kutokana na sababu ya viwanja na kutozingatia taratibu za michezo, lakini sababu za kukaa nje kwa muda mrefu inategemeana na jeraha husika na mahitaji ya mchezaji kuzingatia ushauri wa wataalamu ili kupona mapema.
"Kwanza lazima iwepo elimu ya afya ya kujua kila jeraha lina muda wake wa kupona, mahitaji ya mchezaji mwenyewe kuzingatia kikamilifu maelekezo anayopewa akizingatia ni rahisi kupona mapema, anatakiwa kujua ni aina gani ya lishe anapaswa kuitumia, kupumzika na vitu vinavyohusiana na kupona kwake," alisema daktari Gilbert na kuongeza;
"Kuna mazoezi kabla ya mechi na baada ya mechi, lazima wazingatie ni vyakula gani wanapaswa ili kulinda afya na nguvu ya mwili, mfano mchezaji kaumia na hana mlo mzuri wa protini lazima atachelewa kupona kwani mwili wake utakuwa dhaifu, yapo mambo mengi kitaalamu, kikubwa elimu zaidi ni muhimu sina maana hawana,"
"Hayo ni mambo yanayochangia wachezaji kuumia, lakini kukaa muda mrefu inaweza kuwepo sababu nyingine zinazochangia lakini hizi ni baadhi," alisema.