Wanyonge wa Twiga Stars watamba Afrika

Muktasari:
- Fainali za Awcon 2022 zimepangwa kufanyika Morocco kuanzia Julai 2 hadi Julai 23 mwaka huu na zitashirikisha jumla ya timu za taifa za wanawake 12 zitakazogawanywa katika makundi matatu yenye timu nne kila moja.
Timu mbili zilizofungwa na timu ya taifa ya Tanzania ya Wanawake 'Twiga Stars' kwenye mashindano ya soka kwa wanawake ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (Cosafa) zimefanikiwa kuwa miongoni mwa timu za taifa 12 zilizofuzu fainali za soka za Afrika kwa wanawake (Awcon) zitakazofanyika Morocco mwezi Julai.
Wakati Twiga Stars ambayo ilitwaa ubingwa wa Cosafa kwa wanawake mwaka jana ikishindwa kwenda Awcon, vibonde wake wawili iliopata ushindi dhidi yao kwenye mashindano ya soka kwa wanawake Kusini mwa Afrika, Zambia na Botswana zimetinga Awcon.
Wanyonge hao wawili wa Twiga Stars kwenye Cosafa ambao wamefuzu Awcon ni Zambia na Botswana.
Katika mashindano ya Cosafa ya wanawake, Twiga Stars iliifunga Botswana kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya hatua ya makundi na iliichapa Zambia kwenye hatua ya nusu fainali kwa mikwaju ya penati 3-2 baada ya kutoka nayo sare ya bao 1-1.
Lakini baadaye Twiga Stars ilishindwa kufuzu Awcon baada ya kutolewa na Namibia kwa kuchapwa jumla ya mabao 5-3 kwenye mechi mbili za nyumbani na ugenini kwenye raundi ya kwanza ya mashindano ya kuwania kufuzufainali hizo.
Zambia imeowaondosha wababe wa Twiga Stars, Namibia kwa faida ya bao la ugenini baada ya timu hizo kupata matokeo ya jumla ya sare ya bao 1-1 kwenye mechi mbili za nyumbani na ugenini.
Botswana pia imenufaika na kanuni ya bao la ugenini dhidi ya Zimbabwe baada ya kupata matokeo ya jumla ya mabao 3-3. Katika mechi ya kwanza nyumbani, Botswana ilifungwa mabao 2-0 lakini juzi Jumatano ikaibuka na ushindi wa mabao 3-1 ugenini uliowafanya wasonge mbele.
Kutinga kwa Zambia na Botswana kumefanya kutimia kwa idadi ya timu 12 zitakazoshiriki mashindano hayo.
Timu hizo 12 za taifa za wanawake ambazo zimejihakikishia tiketi ya Awcon ni wenyeji Morocco, Uganda, Nigeria, Cameroon, Burkina Faso, Zambia, Botswana, Afrika Kusini, Burundi, Togo, Tunisia na Senegal.