Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanasoka wa Uingereza na maisha ya ushoga, unafiki

Justine Fashanu

Muktasari:

  • Katika kusimamia sheria, taratibu na maelekezo ya mahali pale, macho hayana pazia, sikuamini nilichokiona, kwani wanamichezo wanaume, wakiwamo wanasoka, tena wale tunaowaona kwenye televisheni walikuwa wakiingia mle ndani.

MIONGONI mwa shughuli zangu ninazoruhusiwa kuzifanya hapa Uingereza katika muda wa ziada, ni ubaunsa.

Ni eneo langu la kujidai kwa sababu ya uwezo niliojaliwa kiasili, lakini pia nikaja kupenda baadaye kwa vile huwa ni mtu ninayetaka kuona utii wa sheria ukifuatwa.

Ndiyo maana niliamua kuwa na leseni ya ubaunsa (door supervisor).

Kwa hiyo nilipotoka likizo nyumbani Tanzania hivi karibuni na kurejea London, nilikuwa bado na muda wa kupumzika, hivyo sikurudi moja kwa moja kwenye ajira yangu ya kudumu.

Basi nilipowasiliana na wakala wa kazi ili nipate japo saa chache nijichumie senti (pence) mbili tatu, nilielekezwa klabu ya maraha ya Soho Square.

Huko kulikuwa na hafla iliyoshirikisha jamaa wa aina fulani –  mashoga. Mie nilikuwa mlangoni, kilichoendelea ndani msiniulize.

Katika kusimamia sheria, taratibu na maelekezo ya mahali pale, macho hayana pazia, sikuamini nilichokiona, kwani wanamichezo wanaume, wakiwamo wanasoka, tena wale tunaowaona kwenye televisheni walikuwa wakiingia mle ndani.

Itoshe tu kwa utangulizi huo, sasa tuuangalie mchezo wa soka kuhusiana na suala hilo la ushoga na kukubalika au kukataliwa kwa mashoga mchezoni.

Mchezo unaotambulika kuwa mahiri na maarufu zaidi duniani ni huo wa soka, una fedha nyingi na watu lukuki hutumia muda wao kuufuatilia wakitumia au kutengeneza fedha. Ni mchezo wa wanaume.

Wapo wachezaji wanawake na mashabiki wengi wanawake siku hizi, lakini mazingira yanaonyesha wazi kwamba hilo si eneo lao, pengine hujawa tabia za kiume, kiburi, fujo na hata wanawake au mashoga kudharauliwa.

Ilivyokwishajengeka sasa ni kwamba suala la ushoga kwa wachezaji ‘limefungiwa vioo’ kwa muda mrefu na inavyoonekana kwa tathmini ya Uingereza, halina nafasi kwenye soka.

Februari 2013, mwanasoka wa Marekani, Robbie Rogers, aliyewahi kuchezea klabu ya Leeds alivunja ukimya akajitokeza wazi kujitangaza kwamba yeye ni shoga, lakini alifanya hivyo baada ya kuachana na soka.

Kwake, mawili hayo yalikuwa lazima yaende pamoja. Haingeweza kufikirika kwake kuendelea na kazi yake ya soka akiwa hapa Uingereza, kwa nini?

Walau wachezaji wanane wa soka la kulipwa Uingereza, wamefungua nafsi zao na kuwaeleza washirika wao kwamba wao ni mashoga, lakini wanashindwa kujitokeza mbele ya umma kueleza ukweli huo, wakiogopa mshindo utakaowapata kutoka kwa mashabiki.

Ukweli ni kwamba, mashabiki wa soka wanatambulika kwa tabia zao za kikatili wakati fulani wakifuata mkumbo; wana kawaida ya kuwa na msimamo mkali kuhusu tofauti au udhaifu wa mchezaji yeyote, na kuzitumia kwa manufaa yao wenyewe.

Siku zilizopita, mashabiki waliokuwa na tofauti na wachezaji, walitambulika kutumia masuala yanayohusiana na rangi au asili ya mchezaji kuwapiga chini ya mkanda, na wengine bado hufanya hivyo sasa.

Mwanasoka shoga, katika muktadha huu, atawindwa na kuwa shabaha ya kushambuliwa na hata kutukanwa kutokana na jinsi alivyo.

Mwaka 1990 mshambuliaji wa zamani wa Norwich na Nottingham Forest, Justin Fashanu alijitokeza na kujitangaza wazi kwamba yeye ni shoga, lakini miaka minane baadaye alijiua akiwa na umri wa miaka 37.

Fashanu alikuwa mwanasoka mweusi aliyekuwa akilipwa vizuri kutokana na ujuzi wake kwenye soka uliokwenda na matakwa ya wakati. Hata hivyo, umahiri wake kisoka ulipoanza kudidimia, wachezaji wenzake na viongozi wa klabu yake walitumia kigezo cha ushoga wake kuwa ndiyo sababu ya udhaifu uliompata.

Mawazo yangu ni kwamba, hali hiyo haitakiwi kutazamwa jinsi hiyo, kwa sababu huu ni mwaka 2013 wala si 1413 na tunatakiwa, hata kama sivyo, tuwe tumestaarabika.

Wasakata soka wanatakiwa wahukumiwe kutokana na uwezo wao kisoka uwanjani au udhaifu wao, lakini si rangi wala jinsi yao.

Tumeona kwamba wanasoka wanane wamewaeleza rafiki zao kwamba wao ni mashoga na si ajabu wapo wengine zaidi; lakini hata hao wanane wanaogopa sana kujianika wazi jinsi yao ya kufanya mapenzi, wanaogopa kuwa wazi.

Jason Collins ambaye ni mwanamichezo mahiri wa mpira wa kikapu nchini Marekani, hivi karibuni alikuwa mchezaji wa kwanza wa kulipwa katika ligi ya Marekani kuweka bayana kwamba yeye ni shoga.

Aliungwa mkono na kupewa moyo na uongozi mkuu wa nchi hiyo, yaani Rais Barack Obama.

Robbie Rogers alipoweka wazi hali yake ya ushoga, wachezaji na mashabiki walimuunga mkono kupitia mtandao wa jamii wa Twitter, lakini ulikuwa uungwaji mkono kidogo, lakini pia alishaacha kucheza soka ya kulipwa Uingereza.

Nchini Uingereza, wachezaji hao wanane wanaojulikana kwa wachache kuwa mashoga walimwendea Mwenyekiti wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa Uingereza na kujadiliana naye juu ya ama kujitangaza wazi au la. Saba kati ya hao wameogopa kabisa mrejesho utakaopatikana kutoka kwa mashabiki. Ni kwa sababu ushoga haukubaliki.

Nikiangalia tena kwa Justin Fashanu, nahisi kwamba bado hawa wanasoka wote wanane wanatakiwa si tu kuhofia mashabiki, bali pia kuziogopa hata klabu zao kwa vile jambo hilo ni gumu kukubalika kimaadili.