Wagosi sasa bado moja tu

Muktasari:

  • Mabingwa hao wa zamani wa Bara, inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na alama 26 sawa na KMC nafasi ambayo itaifanya kucheza hatua ya mtoano endapo itamaliza hapo.

MBEYA. WAGOSI wa Kaya, Coastal Union ya Tanga wanazidi kujiimarisha kipindi hiki baada ya kutoka mapumziko wakati timu nyingine wachezaji wakiendelea na mapumziko huko Tanga unaambiwa hakuna kulala.

Mabingwa hao wa zamani wa Bara, inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na alama 26 sawa na KMC nafasi ambayo itaifanya kucheza hatua ya mtoano endapo itamaliza hapo.

Katika michezo mitano iliyosalia kwa Coastal kumaliza msimu huu, michezo miwili ndio itacheza ugenini huku iliyosalia akikipiga nyumbani Uwanja wa Mkwakwani.

Aprili 9 itakuwa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri na baada ya hapo itarejea nyumbani kucheza michezo mitatu na itakapochanga vyema karata zake basi zitamtoa eneo hilo la hatari na mechi hizo ni dhidi ya Mtibwa Sugar Aprili 23, Ihefu Mei 14, Azam FC kisha itafunga msimu kwa kuifuata Simba Mei 28, Uwanja wa Uhuru.

Katika michezo ya duru la kwanza Coastal ilipoteza michezo yote dhidi ya wapinzani wake hao, akilala 1-0 kwa Dodoma Jiji, 2-1 kwa Ihefu, 3-2 kwa Azam na kuchapwa 3-0 mbele ya Simba.
Kocha wa Coastal, Fikiri Elias alisema ratiba imewakaria vizuri na endapo watafanikiwa kupata alama tatu mbele ya Dodoma basi itawafanya kupunguza presha.

"Michezo mitatu unakuwa nyumbani kati ya mitano hiyo ni faida kubwa kwetu kama tutajipanga vizuri sababu mchezo wa mwisho tutakua ugenini wakati ile ya nyumbani tumemaliza. Kama tutafanya vizuri michezo mitatu ya nyumbani itatuhakikishia alama 15 ambazo zitatufanya kupanda nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo na kukwepa kushuka daraja," alisema Elias.

Tangu ipande Ligi Kuu msimu wa mwaka 2018/19 pamoja na Alliance Coastal Union ilikuwa moja ya timu tishio kwenye Ligi Kuu lakini misimu hii ya sasa imeonekana kuchechemea.