Wageni Yanga, Simba kizungumkuti

Muktasari:

Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengi ya michezo yalisimamishwa na serikali kuanzia mwezi Machi mwaka huu ikiwa ni hatua mojawapo ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya Corona.

WAKATI mwanga wa Ligi Kuu Tanzania Bara kurejea ukianza kurejea, hatima ya wachezaji na makocha wa kigeni waliorudi katika nchi zao kumalizia mechi zilizobaki imebaki kwenye mabano.
Licha ya idadi kubwa ya wachezaji na maofisa wa benchi la ufundi wa kigeni kuwepo hapa nchini, baadhi ya nyota walirudi makwao kwa mapumziko yaliyotokana na ligi kusimamishwa na serikali kutokana na tishio la virusi vya Corona.
Hata hivyo kitendo cha kufungwa kwa mipaka kwenye nchi mbalimbali duniani pamoja na shughuli za usafirishaji, klabu hasa za Simba na Yanga zipo shakani kuwakosa waajiriwa wao hao katika mechi zilizosalia.
Kocha wa Yanga, Eymael alieleza kuwa maisha bila kufanya majukumu yake ya kufundisha soka yamekuwa magumu kwani anatamani hata kesho kurudi Tanzania lakini hilo linashindikana kutokana na serikali kuzuia ndege kutoka nje.
"Uongozi Yanga umekuwa ukinihangaikia katika kupata utaratibu na kuweza kurudi Tanzania kwani huku kwetu Ubelgiji kuna baadhi ya mambo yameruhusiwa kufanyika kama Wananchi kuendelea na majukumu yao," alisema Eymael.
Ofisa Mtendaji mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa amesema kwanza wataangalia njia ya kuweza kuwarudisha wachezaji wao wanne
waliokuwa nje ya Tanzania lakini kama litashindikana hilo watacheza bila ya uwepo wao.
Senzo alisema,"tutaangalia ya mambo ya nje kama itakuwa imetoa ruhusa kwa ndege kuingia nchini kutoka katika nchi nyingine na ambacho kinafuata kama kuwaweka wachezaji wetu karantini na kupata vipimo
lakini kama ikiwa tofauti na hivyo tutajua la kufanya pia".
Anasema kama watakosekana wacezaji hao itakuwa ni kama vile wangekuwepo ndani ya
timu lakini ni majeruhi hivyo wangetafuta namna ya kuziba mapengo yao.
 "Tunasubiri tu wakati wa kuanza mazoezi na hapo ligi itakaporudi na tutaanza kufanya mazoezi hata kama wachezaji hao watakosekana.
Wala hatuna wasiwasi nalo kwani tutakuwa na njia mbadala wa kuliziba pengo hili na wala lisionekane," alisema Senzo.
Shirikisho la soka Tanzania (TFF), kupitia kwa Mkurugenzi wa mashindano, Salum Madadi alieleza kuwa wenye mamlaka ya kutangaza kurejea kwa ligi ni viongozi wa juu wa serikali.
"Kwetu tutafanya yale majukumu yetu lakini wenye mamlaka ya namna gani ligi inaweza kurejea na wakati gani hilo si letu bali ni la uongozi wa nchi," alisema Madadi.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Hassan Abbas ameeleza kuwa Ligi Kuu Bara itarejea na hilo halina mjadala, ila kwa namna gani litaelezwa baadaye.
"Ligi itarejea na lazima bingwa wake lazima atapatikana uwanjani," alisema Abbas ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Wachezaji wa Yanga waliokuwa nje ya Tanzania ni kipa Farouk Shikhalo ambaye yupo Kenya, pamoja na Kocha wao mkuu, Luc
Eymael yupo Ubelgiji na kocha wa viungo, Riedoh Berdien ambaye yupo Afrika Kusini.
Kikosi cha Simba wao kinawakosa wachezaji wake wanne ambao kila mmoja yupo nchini kwao na anashindwa kurejea kutokana hakuna
ndege ambayo inaingia hapa kutoka nchi ya Tanzania kutokana na zuio la serikali.
Wachezaji hao wa Simba waliokuwa nje ya Tanzania ni Clatous Chama aliyopo Zambia, Sharaf Eldin Shiboub yupo Sudan, Francis
Kahata aliyekuwepo Kenya na kinara wa mabao wa ligi, Meddie Kagere aliyopo Rwanda.