Wadau: Namungo imethubutu

LICHA ya muujiza pekee ndiyo unaweza kuivusha Namungo kwenye mashindano ya kimataifa, wadau wa soka nchini wamesema timu hiyo imeonyesha uthubutu.

Namungo ambayo leo Jumatano itakuwa nyumbani kuikaribisha Raja Casablanca kuanzia saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam katika mechi za kundi D za Kombe la Shirikisho barani Afrika hata ikishinda itasalia ya mwisho kwenye msimamo wa kundi hilo.

Mpaka sasa Namungo haijaonja ladha ya ushindi kwenye kundi lake, ikisalia na mechi mbili i ikiwamo ya leo, ambazo ni za kuhitimisha ratiba kwani matokeo yoyote hayawezi kuipa nafasi ya kusonga.

Katika kundi hilo, Raja Casablanca inaongoza ikiwa na pointi 12 ikifuatiwa na Pyramids na Nkana zenye pointi sita kila moja na mechi mbili mkononi.

Hata hivyo, Namungo ambayo ina misimu miwili tangu kupanda kucheza Ligi Kuu Bara inashiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza huku kocha mkuu wa timu hiyo, Hemed Morocco akibainisha bado vijana wake wanajifunza.

“Tunapambana huku tukiendelea kujifunza, naamini mechi yetu ya kesho (leo) tutaitumia kuweka heshima nyumbani, tuko vizuri na wachezaji wangu wote watakuwepo kasoro Bigirimana Blaise ambaye ni majeruhi,” alisema.

Hata hivyo, wadau wa soka wamesema licha ya matokeo inayopata Namungo kimataifa, lakini timu hiyo imeonyesha uthubutu.

“Kitendo cha kufuzu makundi ni hatua hasa kwa timu kama Namungo ambao ni wachanga si tu kwenye ligi, pia kimataifa,” alisema Iddi Kipingu, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT).

Kipa wa zamani wa Simba, Mosses Mkandawile alisema Namungo imekosa uzoefu tu kimataifa, lakini imepambana.

“Kama watatulia naamini wanaweza kuwaduwaza Raja Casablanca, binafsi naiona kwenye levo nyingine Namungo kwa misimu ijayo kimataifa kama itaendelea kupata nafasi,”.

Kabla ya kutinga makundi, Namungo ilitoka sare ya mabao 3-3 na Hilal Obayed 3-3 ugenini na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani kisha ikaichapa Al Rabita 3-0 katika mechi za mtoano.