Waandaaji wa pambano la Cheka, Mclntosh wasaka milioni 100

Muktasari:
Pambano hilo limepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Agosti 4, linatarajiwa kuwa la aina yake na Cheka amepania kurudisha adhi yake katika mchezo wa ngumi nchini.
Dar es Salaam. Waandaaji wa pambano la kwanza la ubingwa wa dunia wa uzito wa Super Middle wa Chama cha World Boxing League (WBL) kati ya bondia, Francis Cheka na Muingereza, Daniel McIntosh, Taasisi ya She Can Foundation wanasaka Sh milioni 100 kufikia lengo la kampeni hiyo.
Pambano hilo limepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Agosti 4, linatarajiwa kuwa la aina yake na Cheka amepania kurudisha adhi yake katika mchezo wa ngumi nchini.
Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema wa Viti maalum mkoa wa Mbeya, Sophia Mwakagenda amesema kuwa fedha hizo wanahitaji kwa ajili ya kununua mataulo ya kike wa shule za msingi wa mikoa ya Nyanda za Kuu Kusini.
Mwakagenda ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo alisema kuwa mbali ya kusaka udhamini, pia wanapokea vifaa kutoka kwa wadau mbalimbali ambao watapenda kufanya hivyo.
“Wakati tunataka Cheka ashinde ubingwa huo ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika nchini, pia tunata kuona kampeni hii inafanikiwa, itakuwa kinyume sana kusindwa kufikia lengo na bondia wetu kupoteza pambano, tunawaomba mashabiki wafike kwa wingi na wadhamini wajitokeze pia,” alisema Mwakagenda.
Alisema kuwa mbali ya mabondia hao, pia mabondia wa kike mbalimbali watashiriki katika mapambano hayo.
“Siku hiyo kutakuwa na tamasha kubwa ambalo litashirikisha wanamuziki mbalimbali ambao wataanza kufanya maonyesho yao kuanzia saa 7 mchana, tunaomba wadhamini wajitokeze kudhamini tamasha hili, lengo ni kuondoa kero kwa mtoto wa kike na kuwa na hedhi salama, tunapokea pia vifaa,” alisema.
Alisema kuwa watoto wa kike wengi wanapoteza siku saba za shule kutokana na kukosa mataulo hayo ambayo yangemfanya aendelee na masomo hata kama yupo katika hali hiyo.
Naye Meneja wa Cheka, Beauty Mmari alisema kuwa Cheka amepania kutwaa ubingwa wa chama hicho ikiwa ni mara yake ya kwanza katika historia.
“Hiki ni chama kipya na Cheka ni bondia wa pili kupata nafasi, tumepania kuweka historia kwa kutwaa ubingwa huo, ameanza mazoezi ya gym na amepania kurejesha hadhi yake,” alisema Mmari.