Waamuzi watupwa jela, ZPL yatangaza kiama

Muktasari:
- Hivi karibuni bodi hiyo ilimfungia mwamuzi msaidizi, Mudrick Haji Amour miaka miwili na kutozwa faini ya Sh2 milioni, huku mwamuzi wa kati, Rashid Farhan akila kifungo cha miezi mitatu.
Wakati waamuzi wawili wakifungiwa kuchezesha Ligi Daraja la Kwanza visiwani hapa, Bodi ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) imesema itaendelea kufuatilia mashindano yote ili kuchukua hatua kwa atakayekiuka kanuni.
Hivi karibuni bodi hiyo ilimfungia mwamuzi msaidizi, Mudrick Haji Amour miaka miwili na kutozwa faini ya Sh2 milioni, huku mwamuzi wa kati, Rashid Farhan akila kifungo cha miezi mitatu.
Hatua hiyo ilikuja baada ya waamuzi hao kubainika kutozingatia sheria 17 za soka wakati wa mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza baina ya Taifa Jang’ombe na Inter Zanzibar walioshinda 2-0.
Kwa sasa mashindano yote visiwani hapa yamesimama kupisha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan na ligi zote zitarejea Aprili 28.
Mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Zanzibar, Issa Kassim alisema wakati ligi zikitarajiwa kurejea, hawatamvumilia yeyote atakayekiuka kanuni za mashindano.
Alisema kwa upande wa Ligi Kuu watakuwa makini sana kufuatilia mwenendo wake kuhakikisha viashiria vya upangaji matokeo havitokei na atakayebainika atachukuliwa hatua.
“Tunaenda kuanza mzunguko wa pili, kila timu kwa nafasi yake ijiandae kuliko kutegemea mteremko popote, tutakuwa makini kufuatilia kuanzia Ligi Kuu na madaraja mengine”
“Tunataka kuona ligi yetu ikiisha salama, bingwa apatikane kihalali, tutafuatilia madaraja yote, awe refa, timu au kiongozi atakayehusika na upangaji matokeo atachukuliwa hatua kali,” alisema kigogo huyo.