Viwanja vinne kuwaka moto leo Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, wenyeji Tabora United waliolazimishwa sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania katika mechi iliyopita, leo watapambana na Kagera Sugar ambayo haijaonja ladha ya ushindi katika michezo mitano ya ligi.

MSHIKEMSHIKE wa Ligi Kuu Bara mzunguko wa 23 unaendelea tena leo kwa timu nne kila moja kusaka pointi tatu muhimu kwenye viwanja mbalimbali.

Mchezo wa mapema saa 8:00 mchana utazikutanisha Geita Gold iliyopo nafasi ya 13 na pointi 22 ikiwakaribisha maafande wa Tanzania Prisons walio katika nafasi ya sita na pointi 29, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita.

Timu hizo zinakutana huku zikiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa Oktoba 30, mwaka jana.

Saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, wenyeji Tabora United waliolazimishwa sare ya bao 1-1 na JKT Tanzania katika mechi iliyopita, leo watapambana na Kagera Sugar ambayo haijaonja ladha ya ushindi katika michezo mitano ya ligi.

Tabora iliyoko nafasi ya 14 na pointi 22 baada ya michezo 22 inakutana na Kagera iliyoshika nafasi ya nane na pointi 25 huku ikiwa haijashinda mchezo wowote wa Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho ilipoifunga Ihefu mabao 2-1 Februari 25, mwaka huu.

Kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, wenyeji Namungo waliopo nafasi ya 11 na pointi 23 huku wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 2-0 na Azam FC, watacheza dhidi ya Coastal Union iliyopo nafasi ya nne na pointi zake 33.

Mchezo huo utakaopigwa saa 12:15 jioni, unazikutanisha timu hizo huku Coastal inayonolewa na Mkenya, David Ouma ikitoka kushinda mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu Bara ikianza na bao 1-0 dhidi ya Ihefu kisha 2-1 dhidi ya Mashujaa.

Mchezo wa mwisho baina ya timu hizo kukutana uliopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa, Namungo ilishinda bao 1-0 Septemba 17, 2022, lililofungwa na aliyekuwa nyota mshambuliaji wa kikosi hicho, Reliants Lusajo ambaye kwa sasa anaichezea Mashujaa.

Mechi ya mwisho itapigwa usiku wa leo ambapo Azam FC iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 50 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 55, itawakaribisha 'Wazee wa Mapigo na Mwendo' Mashujaa ambayo inashika nafasi ya 15 na pointi 21.

Mchezo wa mzunguko wa kwanza baina ya timu hizo uliopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika Kigoma, Mashujaa ilichapwa mabao 3-0, Novemba Mosi mwaka jana yakifungwa na nyota wa kikosi hicho, Kipre Junior, Gibril Sillah na Alassane Diao.