Vita ya Mayele, Kagere Kariakoo Derby iko hapa

Vita ya Mayele, Kagere Kariakoo Derby iko hapa

Dar es Salaam. Makali ya safu za ushambuliaji za Simba na Yanga katika siku za karibuni huenda yakaifanya mechi ya watani wa jadi baina ya timu hizo, Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikawa na idadi kubwa ya mabao.

Katika siku za karibuni mechi baina ya timu hizo imekuwa na ukame wa mabao na wastani wa mabao yaliyofungwa kwa mchezo baina ya timu hizo imekuwa haizidi moja. Takwimu zinaonyesha katika mechi tano zilizopita ni mechi moja ambayo ilikuwa na zaidi ya bao moja ikiwa ni ile iliyochezwa Novemba 7, 2020 ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Baada ya hapo, mechi nne zilizofuata hazikuwa na mabao ambapo moja ilimalizika kwa sare tasa - ile ya Kombe la Mapinduzi iliyochezwa Januari 13, mwaka huu ambayo Yanga iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 4-3, nyingine tatu zikimalizika kwa matokeo ya ushindi wa bao 1-0.

Mechi hizo moja ni ya Ligi Kuu mzunguko wa kwanza msimu uliopita ambayo Yanga ilishinda kwa bao 1-0, ikafuatiwa na mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam ambayo Simba iliibuka na ushindi na mechi nyingine ni ya Kombe la Ngao ya Jamii ya kufungua msimu huu ambayo Yanga ilipata ushindi wa bao 1-0.

Hata hivyo kasi ya kufumania nyavu ambayo timu hizo zimekuwa nazo katika siku za hivi karibuni inatoa ishara kuwa huenda namba ya mabao ikaongezeka katika mechi baina ya timu hizo itakayochezwa Disemba 11 ikiwa ni ya mzunguko wa kwanza katika Ligi Kuu msimu huu.

Timu hizo katika michezo mitano iliyopita zimekuwa na takwimu bora za kufunga bao angalau katika kila mchezo tofauti na zilivyoanza msimu huu. Katika mechi hizo za mashindano mbalimbali iliyoshiriki, Simba ambayo ni mwenyeji wa mchezo huo imepachika mabao 10 ambayo ni wastani wa mabao mawili katika kila mchezo.

Ni kama ilivyo kwa Yanga ambayo katika mechi tano zilizopita ambazo imecheza katika Ligi Kuu, imefunga jumla ya mabao 10 ikiwa ni wastani wa mabao mawili katika kila mchezo.

Wakati Simba ikiingia katika mchezo huo ikiwategemea zaidi Meddie Kagere aliyefunga mabao manne kwenye Ligi Kuu hadi sasa, Yanga yenyewe itamtegemea zaidi Fiston Mayele na Feisal Salum ambao kila mmoja amefunga mabao matatu.

Hata hivyo nyota wa zamani wa timu hizo wameliambia gazeti hili kwa nyakati tofauti kuwa pamoja na kasi ya kufunga mabao kwa timu hizo kwenye mechi tano zilizopita, mechi ya watani inaweza kutokuwa na mabao mengi kama ilivyotokea kwenye mechi baina ya timu hizo hivi karibuni.

“Yanga ipo vizuri, lakini kwenye mchezo huo, lazima wachezaji wajitoe kuhakikisha mashabiki wao wanaondoka kwa kicheko, kuhusu safu za ushambuliaji zipo vizuri kwa pande zote mbili,”alisema nyota wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema kuwa haamini kama mechi hiyo itakuwa na mabao mengi.