Vipigo timu za Taifa vyamchosha Rais Samia

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan leo kwa mara ya kwanza amelihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Machi 19, 2021

Matokeo yasiyoridhisha ya timu za taifa za soka za Tanzania yanaonekana kumkwaza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan aliyesema amechoshwa kuona zikiwa zinafanya vibaya.

Akizungumza wakati wa kulihutubia Bunge leo huko Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan alisema serikali itahakikisha inatoa sapoti kubwa kwa sekta ya michezo ili iweze kupiga hatua na kuitangaza vyema nchi.

Miongoni mwa sapoti hizo ni kuweka bajeti maalum ya fedha kwa ajili ya kusaidia uendeshaji wa timu hizo zile za wanaume hadi wanawake.

"Tutatenga fedha kwa ajili ya kuziandaa timu zetu za taifa zikiwemo za wanawake. Tumechoka kuitwa lile jina aliloliita Mzee Mwinyi (Ali Hassan). Nasi tuingia kwenye ramani ya wacheza 'football' (mpira wa miguu)," alisema Rais Samia.

Ikumbukwe kwamba hii ni mara ya pili kwa serikali kuahidi bungeni, kutenga fungu la kuzisaidia timu za Taifa.

Kabla ya Rais Samia, mtangulizi wake, Hayati John Magufuli naye aliahidi jambo kama hilo wakati walipolihutubia Bunge mwaka jana.