Vigogo wa Coastal wameamua, waanza na uwanja

Muktasari:

  • Coastal Union imefuzu nusu fainali ya kombe la shirikisho, ambapo inatarajia kukutana na Azam kusaka nafasi ya kutinga fainali, huku kwenye Ligi Kuu ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 32.

Mwenyekiti wa Klabu ya Coastal Union, Steven Mguto amesema wanatarajia kuanzia Agosti, mwaka huu, wataanza kutumia uwanja wao kwa ajili ya mazoezi, huku akieleza kuwa msimu huu wanaitaka nne bora na taji la Kombe la Shirikisho (FA).

Coastal Union imefuzu nusu fainali ya kombe la shirikisho, ambapo inatarajia kukutana na Azam kusaka nafasi ya kutinga fainali, huku kwenye Ligi Kuu ikiwa nafasi ya nne kwa pointi 32.

Akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa klabu hiyo uliofanyika jijini hapa, Mguto amesema tayari wameshasafisha eneo lote la uwanja na kinachoendelea ni vipimo kulingana na vigezo vinavyotakiwa.

“Mradi wa uwanja mpaka sasa unaendelea vizuri, tumemaliza kusafisha eneo lote la ‘pitch’ na kilichobaki ni kufanya vipimo na matarajio yetu tutaanza kuutumia kwa mazoezi Agosti, mwaka huu,” amesema Mguto.

Mguto ameongeza kuwa msimu huu wanaitaka nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, lakini wakitaka kubeba taji la FA ili kufikia malengo yao ya kucheza kimataifa mwakani.

"Nia na madhumuni yetu ni kucheza fainali kombe la shirikisho, lakini tunapambania nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu na tunaweza kufikia malengo hayo na kuwakilisha nchi kimataifa,” amesema kigogo huyo.

Kuhusu usafiri wa timu hiyo, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Omary Ayoub amesema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho na benki moja nchini ili kupata basi la mkopo.

"Tupo katika mazungumzo ya mwisho na benki kutupa basi kwa mkopo na suala hili litakamilika ndani ya miezi mitatu, hivyo niwaombe mashabiki kuwa na subira,” amesema Ayoub.