Vigogo Kikapu vitani NBL

Muktasari:

Bingwa wa NBL atafuzu kucheza mashindano ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (BAL) 2021, msimu huu timu ya JKT ndiyo pekee imefuzu kucheza raundi ya pili ya BAL itakayoanza baadae mwezi huu huku timu za wanawake za  JKT na Don Bosco zikishindwa kutamba sanjari na Oilers kwa wanaume.

NANI atatinga fainali ya Ligi ya Taifa ya  Kikapu (NBL)? Ndilo swali linalowapasua vichwa mashabiki wa mchezo huo, lakini kitendawili hicho  kitatenguliwa jioni ya leo wakati vigogo wa wanne watawasha moto kwenye mechi za nusu fainali.
Savio itavaana na Pazi katika nusu fainali ya kwanza wakati JKT ikicheza na Oilers kuanzia saa 12 jioni kwenye uwanja wa Ndani wa Taifa, Dar es Salaam.
Savio yenye rekodi ya kutwaa ubingwa wa RBA mara kadhaa itakutana na Pazi ambayo imekuwa ikiipa ushindani kwenye RBA.
Timu zote hizo zimetinga hatua ya mtoano wa RBA itakayoendelea wiki ijayo ambapo JKT imemaliza ikiwa kinara katika msimamo Oilers ni ya tatu, Savio ya nne ikiwa na pointi 52 katika michezo 30 ambapo imeshinda 23 na kufungwa saba.
Pazi haijafuzu kucheza mtoano kwenye RBA ila kwenye msimamo ni ya tisa ikiwa na pointi 43 katika mechi 16 ilizoshinda huku vinara JKT ikiwa imeshinda michezo 28 kati ya 30 na Oilers michezo 23 sawa na Savio katika RBA.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Kikapu Tanzania (TBF), Manase Zabron alisema mashindano hayo yatafungwa kesho Jumamosi na bingwa ataondoka na kombe na medali.
"Ushindani ulikuwa mkali, timu zote ziko vizuri na hakuna shaka bingwa wa NBL msimu huu anapaswa kufanya kazi ya ziada," alisema Manane akibainisha kwamba timu 14 kutoka mikoa mbali mbali nchini zilishiriki ligi hiyo kwa wanaume.
Upande wa wanawake, DB Lioness, Vijana Queens, Ukonga Queens na Deep Sea Queens ya Tanga zinachuana katika mtindo wa Ligi kusaka bingwa.