Valentin Nouma atambulishwa rasmi Simba SC

Muktasari:
- Nouma mwenye umri wa miaka 24 anakwenda kuiongezea Simba nguvu upande wa kushoto akisaidiana na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambapo msimu uliopita alikuwa pekee katika nafasi hiyo, japo David Kameta 'Duchu' ambaye ni beki wa kulia alisajiliwa kwa nia ya kumsaidia na kutumika mara chache mno.
KLABU ya Simba imemtambulisha beki wa kushoto mpya raia wa Burkina Faso, Valentin Nouma akitokea timu ya St. Eloi Lupopo ya DR Congo kwa mkataba wa miaka mitatu.
Nouma mwenye umri wa miaka 24 anakwenda kuiongezea Simba nguvu upande wa kushoto akisaidiana na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ambapo msimu uliopita alikuwa pekee katika nafasi hiyo, japo David Kameta 'Duchu' ambaye ni beki wa kulia alisajiliwa kwa nia ya kumsaidia na kutumika mara chache mno.
Nyota huyo aliyewahi kuwa Mchezaji Bora wa msimu wa 2022/23 akishinda tuzo ya Beki Bora wa mwaka katika Ligi ya Burkinafaso enzi akiichezea klabu ya AS Douanes.
Ubora mwingine aliokuwa nao Nouma ni kufunga kwa kutumia mipira ya adhabu pamoja na uwezo mkubwa wa kufunga mikwaju ya penalti. Msimu uliopita Simba ilimtegemea zaidi Saido Ntibazonkiza kwenye mipira ya penalti sambamba na Clatous Chama ambao wote wameachwa na klabu hiyo. Chama akitua Yanga.
Simba imekuwa ikiimaisha kikosi kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano wa 2024-2025 ikiongeza sura za kazi katika kila idara ili kuwa na wachezaji wenye viwango vya hali ya juu watakaoweza kupambana katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Nouma anakuwa mchezaji wa 10 mpya kutambulishwa na Simba baada ya Steven Mukwala, Augustine Okenjepha, Charles Ahoua, Joshua Mutale, Debora Fernandes ambao ni wageni, huku wazawa wakiwa ni wanne, Valentino Mashaka, Lameck Lawi, Abdulrazak Hamza na Omary Omary.