Uwanja Simba Bilioni 30

Muktasari:

  • Ujenzi wa uwanja mpya  wa Simba unatarajia kugharimu  Bilioni 30 za kitanzania.

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Murtaza Mangungu amesema Uwanja wa Mo Simba Arena unatarajia kugharimu takribani Bilioni 30.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo wakati wa uzinduzi wa kampeni za kuchangia Uwanja huo, Mangungu amesema ni jambo zuri kuwa na Uwanja wao.

“Jambo hili sio geni kwa kuchanga kwa sababu hata slogani yetu ni Simba nguvu moja, makadirio ya Uwanja huu ni takribani Bilioni 30,” amesema Mangungu.

Mangungu amesema Rais wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ameshaanza kwa kuchangia Sh2 bilioni na pesa hizo sio sehemu ya uwekezaji wake.

“Pesa hizi bilioni mbili zilizonza kuchangiwa na Mo Dewji lakini hazihusiani na zile za uwekezaji, lengo tujege uwanja wetu,” amesema Murtaza na kuongeza;

“Inawezekana kuzuiliwa kwa CEO wetu na baadhi ya viongozi kuingia kwenye mechi (Simba na Yanga) kumechangia mashabiki watake tuwe na Uwanja wetu.”

Naye Mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez amesema anashukuru kwa Rais wa klabu hiyo Mohammed Dewji kuchangia ujenzi wa Uwanja .

“Tumepigiwa simu nyingi sana na leo tumeamua kuzindua rasmi kampeni zetu kuhusu Uwanja huu, tunajua Simba wana nia ya kuchangia uwanja wao,” amesema Barbara.

Barbara amesema ;” Kwasasa kamati imekaa na bodi kwa ajili ya michoro ya ramani, mwezi wa kwanza michoro rasmi itatoka.”

Uwanja wa Simba unatarajia kuingiza watu sio chini ya elfu thelathini (30000).
Wanachama na wapenzi wa klabu ya Simba wanachangia kupitia mitandao ya simu pamoja na benki.