Utalii Cup kinawaka Nyamagana, Copco yaishushia Alliance kipigo
Muktasari:
- Mashindano hayo maalum kwa ajili ya kuzipa maandalizi timu za mkoa wa Mwanza kabla ya kuanza msimu mpya yanashirikisha timu za Pamba, Alliance, Copco Veterani, Mbao, Mapinduzi na Jembele FC ya Zanzibar
Mwanza. TIMU ya Copco Veteran imeanza vyema mashindano maalum ya kujiandaa na msimu kwa timu za jiji la Mwanza yaliyopewa jina la Utalii Cup baada ya kuichapa Alliance bao 3-0.
Copco Veteran ambayo imepanda daraja kwenda Championship imeibuka na ushindi huo leo Jumatano katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano hayo uliopigwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Ikiwa inatumia michuano hiyo kutesti baadhi ya vifaa vyake vipya ilivyovuna kwenye kliniki maalum iliyoiandaa kuanzia Julai 12-28 mwaka huu, Copco imepata bao la kuongoza mnamo dakika ya 38 likifungwa na Juma Nade kwa shuti kali na kuifanya iende mapumziko ikiongoza 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kila timu kufanya mabadiliko machache kuongeza nguvu ambapo Copco imeendelea kutawala mchezo huo ikicheza soka la kuvutia na kulifikia lango la Alliance mara kwa mara.
Copco imepata bao la pili dakika ya 53 baada ya beki wa kulia wa Alliance, Brighton Masole kujifunga wakati akijaribu kuokoa krosi iliyomiminwa na Agustino Athanas.
Wakali hao wapya wa Championship walipata bao la tatu mnamo dakika ya 55 likifungwa kwa kichwa na Seleman Seif kwa kichwa baada ya kuwachambua mabeki na kudonoa mpira uliompita kipa na kugonga mwamba kisha akaumalizia kwa kichwa.
Dakika 90 za mchezo huo zimemalizika kwa Copco Veterani kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku Kocha Mkuu wa timu hiyo, Feisal Hau akieleza kuwa michezo hiyo itawa kupata kikosi kizuri kitakachoshiriki Championship ambapo ametumia mchezo wa leo kuwajaribu baadhi ya wachezaji wake wapya aliowasajili.
Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo amesema michuano hiyo ni kipimo sahihi kwa timu za mkoa huo kujiandaa na kuangalia wachezaji wapya ili kuimarisha vikosi vyao.