Ushuhuda wangu kwa mbwana Samatta -3 Katumbi alimpa dili la Ufaransa
Muktasari:
Alikuwa anaishi peke yake. Alikuwa na mfanyakazi wake wa kike wa kizungu raia wa Slovakia. Huyu dada ndiye aliyekuwa anampikia, anamfulia, na kusafisha nyumba. Alikuwa anakuja nyumbani kwa Samatta kufanya kazi siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
HUU ni mwendelezo wa ushuhuda unaotolewa na Edo Kumwembe, mwandishi wa kwanza wa Tanzania kumtembelea mshambuliaji mpya wa Aston Villa ya Ligi Kuu ya England, Mbwana Samatta aliposajiliwa na TP Mazembe ya DR Congo na baadaye KRC Genk ya Ubelgiji. Endelea...
Januari 2016, Samatta aliipa mkono wa kwaheri klabu ya TP Mazembe na kusaini katika klabu Genk ya Ubelgiji. Uhamisho huu ulikuja baada ya maombi mengi na sala za Watanzania za kumtaka Samatta akacheze soka la kulipwa Ulaya baada ya kutamba sana Afrika.
Kilicho nyuma ya pazia ni kwamba, Samatta aliondoka Mazembe kwa kulazimisha kwa sababu tajiri wa Mazembe, Moise Katumbi hakutaka kumuuza. Mkataba wake ulikuwa umebakiza miezi mitano tu umalizike Mazembe na Samatta alikuwa amegoma kusaini mkataba mpya.
Ilipofika mahala ambapo Katumbi aliona hawezi kumzuia Samatta kwenda Ulaya, akaamua kumlazimisha kwenda Ufaransa. Hata hivyo, Samatta na wakala wake wakalazimisha kwenda Ubelgiji katika klabu ya Genk. Sifahamu sababu zao za kulazimisha dili hili.
Kama kawaida, kiherehere changu kilinifanya niwe mwandishi wa kwanza wa Tanzania kwenda mpaka Genk kwa ajili ya kufanya mahojiano na Samatta. Bahati iliyoje. Baada ya kuwa wa kwanza Congo, sasa hivi nilikuwa wa kwanza Ubelgiji.
Nilisafiri kuanzia Dar es Salaam hadi Uswisi, kisha hadi Ubelgiji. Nikafika katika jiji la Brussels kule Ubelgiji na kuweka kituo kimoja kwa rafiki yangu Mrundi anayeitwa Bruno. Huyu ana uraia wa Ubelgiji. Aliwahi kuwa beki wa timu ya taifa ya Burundi na klabu ya kwao ya Vitalo.
Bruno alinipa historia ya muda mrefu ya soka la Ubelgiji. Wingi wa watu weusi nchini Ubelgiji ulinitisha sana. Sikuamini kama Samatta angeweza kuvuka kikwazo cha watu weusi waliozamia Ubelgiji na waliozaliwa Ubelgiji ambao wanacheza soka.
Bruno alinimbia Samatta angefanikiwa tu kama angekuwa na malengo na nidhamu.
Lakini akaniambia kwamba maisha yatakuwa rahisi kwa Samatta Ubelgjji kwa sababu amekwenda kama mchezaji staa, ambaye ndiye kwanza ametoka kuchukua ubingwa wa Afrika, lakini pia amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa ndani wa bara la Afrika.
Kesho yake nikafunga safari kutoka Brussels hadi Genk nikitumia usafiri wa treni. Nilikuwa nimeshafanya mawasiliano ya kutosha na Samatta na aliniambia jioni ambayo ningefika yeye angekuwa mazoezini na ni bora nifikie katika hoteli inayofahamika kwa jina la Hotel M.
Hotel M niliikuta imejaa na nikafikia hoteli inayofahamika kwa jina la Atlantica. Asubuhi Samatta alinipa anuani yake na nikafika kwake. Apartment zilikuwa za kisasa sana. Unapofika katika apartment ambazo Samatta aliishi Genk unajiuliza, maisha yanataka nini zaidi?
Alikuwa anaishi peke yake. Alikuwa na mfanyakazi wake wa kike wa kizungu raia wa Slovakia. Huyu dada ndiye aliyekuwa anampikia, anamfulia, na kusafisha nyumba. Alikuwa anakuja nyumbani kwa Samatta kufanya kazi siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.
Kitu kilichonishangaza zaidi kuhusu dada ni kwamba, pia alikuwa mshauri wa Samatta katika masuala ya vyakula vya wachezaji. Nilipoongea naye akaniambia ana diploma ya masuala ya upishi. Kumbe ndio maana!
Unajaribu kuwaza, Samatta yule aliyekuwa Mbagala Market leo ana mfanyakazi wa kizungu? Hivi ndivyo maisha yanavyomchukua mwanadamu kutoka hatua moja kwenda nyingine. Ndivyo ambavyo kipaji kinamuhamisha mtu kutoka Newala mpaka New York.
Kwa vile Samatta alikuwa anaishi peke yake, akaomba nihamie kwake kutoka hotelini. Hapo nilijikuta nikiwa karibu na habari zaidi. Wakati huo Samatta alikuwa ana miezi minne tangu atue Genk na bado alikuwa mgeni.
Katika jiji la Genk, Samatta alikuwa Mtanzania pekee. Akaniambia mtu pekee ambaye aliwahi kuongea naye Kiswahili katika jiji la Genk ni mama wa staa wa kimataifa wa Ubelgiji anayekipiga Liverpool, Divock Origi ambaye alikutana naye katika supermarket moja jijini hapo.
Genk ni mji mdogo. Kufikia sasa una wakazi 66,110 tu. Kifupi uwanja wa Old Trafford unachukua mashabiki wengi kuliko jiji la Genk. Kifupi, wakazi wote wa Genk wanaweza kuingia uwanja wa Old Trafford na bado tukaona mapengo uwanjani. Trafford inachukua mashabiki 76,000.
Maisha ya Samatta Genk yalikuwa ya kipweke. Kwa nyakati hizo, yalikuwa ya kipweke mno. Lakini pia yalikuwa maisha ambayo yalimfanya awe mwanasoka wa kulipwa hasa. Wachezaji wengi wa Genk walipenda kuishi katika mji jirani wa Hasselt. Kilomita 20 kutoka Genk.
Pale Hasselt pamechangamka zaidi kuliko Genk. Klabu za usiku, supermarket za kisasa zaidi, kituo cha treni kikubwa zaidi, na mengineyo. Samatta aliniambia aliamua kubaki mji uliotulia wa Genk kwa ajili ya kuiweka akili yake katika mpira zaidi.
Maongezi yetu ya awali yalijikita katika maisha yake ndani ya mwezi wake wa kwanza Genk.
Wakati huo alikuwa na miezi minne Genk na tayari kuna vitu alikuwa ameshavipitia. Lakini maongezi yake ya namna alivyowasili na kuishi katika mwezi wa kwanza yalinifurahisha zaidi. Ilionekana wazi kwamba wenzetu ni watu makini.
Samatta alinieleza jinsi alivyopimwa afya katika hospitali nne tofauti katika jiji la Genk. Walimpima kila kitu. lakini walimpima pia meno. Madaktari watanisaidia hapa jinsi ambavyo meno yalivyo kiungo muhimu katika mwili wa mwanadamu. Jinsi meno yanavyobeba mishipa ya fahamu ya mwili wa mwanadamu.
Baadaye Samatta alinisimulia pia jinsi ambavyo katika siku za mwanzo kocha wake alimpeleka katika timu ya wachezaji wa akiba iliyochanganyika na wachezaji vijana. Sawa alikuwa amenunuliwa kama mchezaji wa timu kubwa, lakini ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza na kuishi Ulaya. Alipaswa kuingia taratibu katika mfumo.
Walikuwa wakicheza mechi nyingi na kwa mujibu wake, alikuwa anafunga mabao mengi kiasi kwamba kocha alilazimika kumrudisha katika kikosi cha kwanza haraka haraka ili aanze kuisaidia timu.
Samatta ananiambia kulikuwa na ‘Samatta watatu’ tofauti katika maisha yake ya soka. Samatta wa Simba, wa TP Mazembe na huyu wa Genk. Anaamini kwamba kucheza Genk kunahitaji utulivu wa hali ya juu pamoja na nidhamu. Kwa mfano, siku ambayo nilikuwa napiga soga hili, usiku wake tulitembea umbali mrefu kwenda kula chakula cha usiku katika mgahawa anaoupenda, na kesho yake Genk walikuwa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya timu ya Oostende.
Itaendelea kesho.