Upande mmoja wa Malinzi na mafanikio ndani ya TFF

Muktasari:

Makala haya yanajaribu kulinganisha na kukubali  wapi Tenga alikuwa mbele na wapi Malinzi amemzidi kete mtangulizi wake huyo.

KUMEKUWAPO na maneno kuhusu utawala wa Rais wa Shirikisho la Soka la Tanzania, Jamal Malinzi. Mjadala unakuzwa na ulinganisho unaofanywa dhidi ya utawala wa mtangulizi wake, Leodegar Tenga.

Katika mjadala huo, baadhi ya wadau wa soka wamekuwa wakisema kiongozi huyu wa sasa ameshindwa na hafai kuendelea kuliongoza shirikisho hilo, wadau hao wanaliangalia hili katika mtazamo wa kiutawala zaidi, kisha wanatoa majumuisho kuwa Malinzi hafai.

Lakini kwa mtazamo wa jicho la ziada, yapo mambo ambayo ukiyalinganisha na utawala uliotangulia wa shirikisho hilo, unaweza kutoa majibu ya hapana.

Makala haya yanajaribu kulinganisha na kukubali  wapi Tenga alikuwa mbele na wapi Malinzi amemzidi kete mtangulizi wake huyo.

Utawala bora wa soka

Hapa ndipo unapoweza kumpa heko Tenga kuwa wakati wake kulikuwa na mpangilio mzuri katika mambo mengi tu yaliyohusu utawala bora. Maamuzi mengi ya kamati zilizoundwa wakati wa Tenga yalikuwa yakitoka kwa uhuru zaidi na hivyo kuwapa nafasi watu waliokutwa na hatia kukata rufaa kwenye ngazi iliyokuwa ikifuata.

Uhuru huo ndio uliompa nafasi hata Malinzi kushinda katika kusudio lililotaka kumtia hatiani ili asije kugombea nafasi aliyonayo. Chaguzi nyingi kuanzia za vyama shiriki vya TFF mpaka vyama vya mikoa zilizofanyika chini ya utawala wa Tenga, zilikuwa zikimalizika kwa amani huku kukiwa hakuonekani nia mbaya ya kupanga safu za uongozi wa juu.

Kwa ufupi ukizungumzia utawala bora, enzi za Tenga ulikuwa unakiona kitu fulani kizuri.

Uhuru wa utendaji kazi wa sekREtarieti ya TFF

Kuna tofauti kubwa ya namna sekretarieti ya Tenga ilivyokuwa ikifanya kazi na hii ya sasa chini ya Malinzi. Ungeweza kuuona uhuru mkubwa waliokuwa nao waliokuwa chini ya Tenga kuliko ilivyo kwa walio chini ya Malinzi.

Enzi za Tenga, watendaji kama Mkurugenzi wa Ufundi, Katibu Mkuu au maofisa wengine wa TFF hawakuwa na mipaka ya maamuzi, mfano wakati wa Kombe la Taifa lililofanyika Tabora, kulikuwa na malalamiko yaliyowafanya Mkurugenzi wa Ufundi wakati ule, Sunday Kayuni, kutofautiana na Katibu Mkuu wake, Frederik Mwakalebela. Ni kwa sababu kila mmoja alijiona yupo sawa.

Haikuwa raisi pia kumpata Rais hata pale ulipokuwa unataka kutoa ushauri, ni kwa sababu kila kitu kilitakiwa kipitie kwa watendaji na hii ilifanya baadhi ya mashauri ya kiufundi kutomfikia Tenga moja kwa moja.

Kwa sasa kuna tofauti. Kila kitu kinachofanyika ndani ya TFF kina uwazi hadi kwa Malinzi. Hii imekuwa na faida hasa pale ushauri unapohusisha na utendaji wa ndani wa shirikisho.

Ujenzi wa Stars kwa kutumia wazalendo

Hili halikuwezekana kipindi cha Tenga baada ya kuachana na kocha mzawa Mshindo Msolla. Kuanzia hapo TFF haikuwaza tena kumtafuta mzalendo zaidi ya kuangalia makocha wa nje ya nchi.

Na hii ilikuja kutekelezwa kwa kasi baada ya Serikali kujitolea kuwalipa mishahara makocha wote wa timu za Taifa, hapa ndipo tulipoanza na Marcio Maximo, Jam Poulsen na Kim Poulsen.

Hatukuweza kutoa nafasi nzuri kwa wazalendo kuingia kwenye ukufunzi wa Taifa Stars kwani hata kwenye timu za vijana, bado TFF chini ya Tenga iliwakumbatia makocha kutoka nje. Ni kipindi hicho na ujio wa kocha wa vijana, Kim Poulsen, uliambatana na ujio wa kocha mwingine wa timu ya vijana chini ya miaka 17, Jacob Mickelsen.

Lakini Jamal Malinzi ameweza kuwaamini wazalendo kuanzia kocha mkuu wa Taifa Stars hadi chini.

Hivi sasa timu za vijana za Tanzania zina makocha wanaohusika nao moja kwa moja na wameajiliwa kwa kazi hiyo huku Salum Mayanga akiwa mzalendo wa pili kuinoa Stars nje ya wazungu wengi waliopita Stars.

Ligi za vijana na wanawake kuchezwa mikoani

Kipindi cha Tenga nchi ilishuhudia michuano mingi ya vijana kuanzia ile ya Copa Coca Cola hadi Airtel Rising Stars bila kusahau Kombe la Uhai kwa vijana chini ya miaka 20, lakini bado utawala huo ulishindwa kuwapa akina dada michuano rasmi.

Ulikuwa ni utawala huo ulioikuta wilaya ya Kinondoni ikiwa na Ligi ya Wanawake,  bahati mbaya uongozi huo ulishindwa kuichukua ligi hiyo na kuipanua angalau kuwa ya kanda na mwisho kuwa ya kitaifa zaidi.

Ilikuwa ni katika kipindi hicho ambako awali nchi ilikuwa na vituo vya vijana wakifanya mazoezi pamoja na shule, mfano sekondari za Makongo na  Jitegemee, DYOC, Elite Soccer School, Emima na vituo vingine. Lakini TFF ya muda huo ilishuhudia vituo hivyo vikipotea taratibu, hakukuwa na utaratibu hata wa kuvipa ruzuku ya vifaa vya kufanyia mazoezi.

Lakini sasa, angalau TFF ya Malinzi imeweza kushirikiana na washirika wengine kama Azam TV kuanzisha ligi kuu ya wanawake ambayo imeshirikisha timu kadhaa za Tanzania na inawezekana hii ikasambaa nchi nzima.

Ujenzi wa timu za Taifa za vijana

Kwa muda wa utawala wa Tenga, kulikuwa na rundo la wachezaji vijana waliopatikana kwenye maeneo ya kujifunzia, ilikuwa ni sehemu tosha ya kuanzia kwa nchi kupata timu za kesho.

Yale ambayo baadhi ya wadau walishauri kuhusu ujenzi wa soka la vijana kipindi hicho na ambayo hayakufuatwa, ndiyo yanayowapa jeuri watawala wa sasa kujitofautisha na waliotangulia.

Ndicho kipindi ambacho michezo shuleni ilikuwa imerudishwa, lakini hakukuwa na ufuatiliaji wa kina wa TFF chini ya Kurugenzi ya Ufundi. Hakukuwa na mikakati iliyoridhisha ya ubunifu kuhusu ujenzi wa soka la vijana.

Kwa sasa hali ni tofauti kiasi. TFF hii inafuatilia uundwaji wa timu za vijana hatua kwa hatua na kuhusika nao moja kwa moja. Ukiacha na jinsi kundi la vijana wa miaka hii chini ya Serengeti Boys lilivyotayarishwa hadi kushiriki michuano hii ya Afrika na kufanikiwa kufikia fainali zitakazochewa Gabon, jinsi wachezaji walivyokuwa wakijumuishwa kila baada ya wiki mbili au mwishoni mwa mwezi kisha kupewa michezo ya kirafiki ndani na nje ya nchi na baadaye kupata mialiko nje ya bara letu, tayari TFF imefanya makubwa kwenye uandaaji wa timu nyingine.

TFF imewaweka pamoja wachezaji waliokuwa na miaka 14 wakisoma huko Mwanza. Ni nafasi ambayo chini ya Tenga, TFF ingeweza kuitumia Sekondari ya Makongo kuwahifadhi vijana na kisha kuwaendeleza katika timu za vijana ambapo baadaye wangekuja kuwa tegemeo la Taifa.

Kwa miaka ya uongozi wa Tenga, lazima nchi hii ingeshakuwa na hazina kubwa ya wachezaji kwa kutumia utaratibu huo.

TFF hii ya Malinzi imejidhatiti kufanikisha hilo baada ya kuwakusanya vijana wa umri chini ya miaka 14 na kuendelea kuwatunza huku wakipata elimu pale Alliance Mwanza. Hawa ndio vijana watakaokuwa tegemeo la kesho.

Ni wazi katika eneo hili ndilo linalompa Malinzi heshima kwani soka pamoja na mambo yote ya kiutawala, nchi kuwa na ligi nzuri na mambo mengine, bado mafanikio makubwa ni kuona timu za Taifa zinashiriki fainali nyingi za michuano mikubwa. Kwa hapa tunaanza kuuona mwelekeo, japo unaweza kusema ni mapema.