Uongozi wa Birdi mbio za magari hatarini

Muktasari:
- Kwa sasa, Gurpal Sandhu wa Arusha ndiye anayeongoza msimamo wa jumla kwa kuwa na pointi 52.
UONGOZI wa Manveer Birdi katika mbio za kusaka taji la taifa la ubingwa wa mbio za magari umepata tishio jipya baada ya kushindwa kumaliza mashindano ya mbio za magari ya Dar es Salaam mwishoni mwa juma.
Kwa sasa, Gurpal Sandhu wa Arusha ndiye anayeongoza msimamo wa jumla kwa kuwa na pointi 52.
Kutokana na Birdi kushindwa kumaliza, Randeep Singh sasa ndiyo tishio jipya baada ya kushinda raundi ya pili na kufungana na Birdi kwa pointi 35.
Matokeo ya raundi ya pili ya ubingwa wa mbio za magari kitaifa, licha ya kuwa na manufaa makubwa kwa mshindi, Randeep Singh pia yamezidi kumsogeza mbele Gurpal Sandhu wa Arusha ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu na Shehazad Munge ambaye amerudi tena mchezoni mwaka huu na kufanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili katika michuano ya mwishoni wa juma. Akiongozwa na msoma ramani Mahmeet Singh ndani ya Mitsubishi Evolution 1X, Randeep alitumia muda wa saa 1, dakika 06 na sekunde 48 kushinda mbio hizo ambazo zilichezwa zaidi katika maeneo ya Kazimzumbwe, Kisura na Sungwi katika wilaya ya Kisarawe.
Nafasi ya pili ilichukuliwa na Shehazad Munge wa Dar es Salaam aliyetumia saa 1, dakika 07 na sekunde 19 akiendesha gari aina ya Mitsubishi Evo X.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Gurpal Sandhu aliyetumia saa 1, dakika 19 na sekunde 15 akiongiozwa na msoma ramani kutoka Zambia, David Sihoka ndani ya gari aina ya Mitsubishi Evo X. Arshi Somji ambaye alishika nafasi ya nne ni alikuwa ni mmoja wa maingizo mapya katika mashindano haya.
Somji, aliyekuwa akiongozwa na msoma ramani Karim Munisi, alitumia muda saa 1, dakika 38 na sekunde 46 akiendesha gari aina ya Subaru Impreza. Magari 7 ndiyo yalifanikiwa kumaliza mashindano wakati magari 4 yakishindwa kumaliza kutokana na hitilafu mbalimbali za kiufundi.
Licha ya Manveer Birdi, madereva wengine walioshindwa kumaliza mbio hizi na pamoja na Dharam Pandya ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu katika raundi ya ufunguzi mjini Iringa, Zubayr Piredina na Tufail Tufail.
Aliyemaliza katika nafasi ya tano alikuwa Zaneal Somji wa Dar es Salaam ambaye alitumia saa 1, dakika 54 na sekunde 51 wakati nafasi ya sita ilichukuliwa na Ismail Tharia aliyetumia 1:58:42.
Timu ya Amapiano ya Charles Bicco na David Matata, ndiyo iliyoshika nafasi ya saba ndani ya gari aina ya Subaru Impreza N12.