Uongozi ngumi za kulipwa wasimamishwa

Muktasari:

  • Habari ambazo Mwananchi Digital imezipa zinaeleza uongozi huo umesimashwa jioni hii ya Mei 8, 2024 mjini Dodoma baada ya kikao cha Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Damas Ndumbaro na wadau wa ngumi.

 Uongozi wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) umesimamishwa kupisha uchunguzi.

Habari ambazo Mwananchi Digital imezipa zinaeleza uongozi huo umesimashwa jioni hii ya Mei 8, 2024 mjini Dodoma baada ya kikao cha Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Damas Ndumbaro na wadau wa ngumi.

Hata hivyo, waziri Ndumbaro alipopigiwa simu, haikupokelewa huku katibu mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Neema Msitha aliyekuwepo kwenye kikao hicho cha Waziri alipopigiwa alipokea na kusema yuko bize apigiwe baadaye.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayay ambaye pia inaelezwa alikuwepo kwenye kikao alipopigiwa alikata simu na kuandika ujumbe mfupi kwamba hawezi kuzungumza muda huo.

Habari kutoka Dodoma zinasema, Waziri Ndumbaro ameuondoa madarakani uongozi huo na kumteua Emmanuel Salehe kukaimu nafasi ya rais, Chaurembo Palasa aliyesimamishwa.

Uongozi huo wa muda pia utakuwa na wajumbe kadhaa akiwamo bondia wa zamani, Patrick Nyembela na mwanahabari, Shafii Dauda.

Palasa alipotafutwa simu yake iliita kidogo na kukatwa ambapo jitihada za kumtafuta bado zinaendelea.