Ule utamu WPL umerudi tena

ULE utamu wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) iliyokuwa imesimama kwa zaidi ya mwezi mzima kupisha michuano ya kimataifa kwa timu za taifa za wanawake, umerudi tena wakati mechi za ligi hiyo zitakapopigwa leo kwenye viwanja vitano tofauti.

Ligi hiyo ilisimama tangu zilipochezwa mechi za mwisho mwanzoni mwa Februari na ilitarajiwa kuanza rasmi duru la pili Machi 12, kabla ya kusogezwa hadi leo Ijumaa ambapo zitapigwa mechi tano za kibabe za kufungulia pazia la duru hilo la lala salama.

Watetezi wa taji, JKT Queens waliomaliza duru la kwanza na mkosi wa kunyang'anywa pointi tano na kutozwa faini ya Sh3 milioni kutokana na ishu ya mechi yao dhidi ya Simba Queens, watatupa karata leo dhidi ya Bunda Queens kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.

Katika mechi ya duru la kwanza baina ya timu hizo, JKT ilishinda ugenini kwa mabao 4-0.

Mechi nyingine zitakazopigwa leo ni ile ya Ceasiaa Queens dhidi ya Simba (Samora, Iringa), Geita Gold dhidi ya Alliance Girls (Nyankumbu, Geita). Katika mechi ya kwanza baina ya timu hizo Alliance ilishinda 2-1 nyumbani, lakini ikaja ikanyang'anywa pointi na kulimwa faini kwa kumchezesha Nelly Kache anayedaiwa hakuwa halali, hivyo mechi ya leo ni ya kisasi kwa timu zote mbili.

Timu ya Amani Queens itacheza dhidi ya Fountain Gate Princess huko Ilulu, Lindi na Yanga Princess itakuwa nyumbani dhidi ya Baobab kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam.

Hadi sasa mbio za ubingwa katika duru hili la pili zipo kwa vigogo, Simba, JKT na Yanga zinazoonekana kuwa na nafasi nzuri kutokana na ushindani wa pointi.

Simba Queens inaongoza msimamo kwa tofauti ya pointi sita juu ya JKT iliyoshushwa kutoka kileleni ikiwa na 19 katika nafasi ya pili, pointi moja juu ya Yanga yenye pointi 18 na nafasi ya nne inashikwa na Ceasiaa Queens yenye pointi 16.

Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi' alisema kwa mandalizi waliyofanya wanaamini duru la pili litakuwa zaidi ya lile la kwanza katika kuwania ubingwa ambao unashikiliwa na JKT.

"Lengo ni kujiweka vizuri zaidi na kuhakikisha mzunguko wa pili tunaendelea kufanya vizuri zaidi ukizingatia mpaka sasa tunaongoza ligi, hivyo tunatakiwa kujiandaa zaidi ili tuje tofauti kwa kufuta makosa yote yaliyojitokeza na tuwe bora zaidi," alisema Mgosi.

Kocha wa Ceasiaa Queens, Ezekiel Chobanka alisema; "Tunapocheza na timu kubwa sisi timu ndogo tunaonekana hatuna uwezo, tuko nafasi ya nne lakini hatujaridhika nayo tutapambana mzunguko wa pili tuingie tatu bora na makosa tuliyofanya hayatajirudia."